Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imemfungia mlango mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe baada ya kukataa kumuongeza katika orodha ya mashahidi wa walalamikaji katika kesi ya uchaguzi inayomkabili mbunge wa wa jimbo hilo Clayton Chipando, maarufu kama Baba Levo (CCM).

Uamuzi huo ulitolewa jana, Ijumaa, Julai 10, 2026 na Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo kufuatia maombi ya walalamikaji kutaka kumuongeza Zitto katika orodha ya mashahidi wao.

Kutokana na uamuzi huo, walalamikaji hao waliamua kufunga kesi kwa upande wao baada ya kuwaita mashahidi 16, waliotoa ushahidi kwenye kesi hiyo, na Mahakama ikapanga kutoa uamuzi wake Julai 16, 2026, kama walalamikiwa wana kesi ya kujibu au la.

Baba Levo alitangazwa mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025,  akimshinda mpinzani wake Zitto Kabwe aliyegombea nafasi hiyo kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.

Kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Baba Levo ilifunguliwa na  wapigakura wanne wa jimbo hilo ambao ni Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo  Kombolela na  Lumu  Mwitu.

Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 mbali na Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili, walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji hao wanadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, vikiwamo vitendo vya rushwa na udini vilivyofanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Jinsi ilivyokuwa

Jana, asubuhi wakili wa walalamikaji, John Seka aliwasilisha maombi katika Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama akiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo ya shahidi muhimu katika kesi hiyo, Zitto.

Maombi hayo yalisikilizwa jioni baada ya kumalizika ushahidi wa shahidi wa 16 na wa mwisho kwa waliokidhi matakwa ya kustahili kutoa ushahidi.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, wakili Seka aliieleza Mahakama kuwa, awali walieleza kuwa wana mashahidi 20; kutokana na changomoto za mfumo wa Mahakama walifanikiwa kuwasilisha maelezo ya mashahidi 16 tu.

Alieleza kuwa, kutokana na kujirudiarudia kwa hoja zinazomhusu Zitto  aliyekuwa mgombea kupitia ACT- Wazalendo wakati wa maswali ya dodoso, wametambua kuwa hakuwa sehemu ya mashahidi hao ni shahidi muhimu.

“Hivyo kwa kuwa ametajwatajwa ni muhimu naye apate fursa ya kusikilizwa ili naye aseme kwa yale aliyokuwa akitajwatajwa kwayo,” alisisitiza wakili Seka.

Alidai kuwa wadau wengine waliotajwa sana ambao ni muhimu ni walalamikiwa watapata fursa ya kusikilizwa  kueleza mazingira ya mambo waliyotajwa nayo isipokuwa Zitto.

Hivyo alidai kuwa, ili kwenda kwenye kiini na kujibu kwa usahihi hoja zilizoko mahakamani wameona ni muhimu kumuita, kwa kuwa  atawasaidia waombaji kupata haki kwa mujibu wa Ibara ya 13(1) na (6)(a) ya kusilizwa na kikamilifu.

Pia, alibainisha kuwa iwapo maombi hayo yatakubaliwa walalamikiwa hawataathirika kwa kuwa watakuwa na fursa ya kumdodosa na kwamba bado nafasi ya waombaji ya Kikatiba na kisheria ya kuleta mashahidi, haijafungwa.

Hivyo alidai kuwa waombaji wanatumia kifungu cha 103 na 105 vya Sheria ya Mashauri ya Madsi (CPC) kuwasilisha maombi hayo, na kwamba wamekidhi masharti yaliyowekwa na Mahakama kuhusu maombi ya namna hiyo ikiwamo kuwa na sababu ya kuridhisha.

Alidai kuwa, kwa kuwa shahidi huyo amekuwa akitajwatajwa wanaona hiyo ni sababu ya msingi.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola alisema wanapinga maombi hayo kwa kuwa tangu Novemba 15, 2025 walalamikaji walipofungua shauri mpaka leo ni miezi minane, walikuwa wanajua kuwa Zitto ni mtu muhimu kwa kuwa walimtaka hata kwenye hati ya shauri.

Pia, alikumbusha kuwa waombaji wameshaomba mahakamani mara mbili  kuongezewa muda wa kuleta maelezo ya hao mashahidi, na kwamba baada ya maelezo ya mashahidi kuwasilishwa mahakamani hakuna mahali ambako kanuni zinatoa mwanya wa kuongeza mashahidi.

Alidai kuwa Kifungu cha 105 (CPC) kinatoa mwanya huo kama kuna jambo la haki na kwamba imewaongezea muda huo mara mbili, huku  akidai kuwa, kifungu hicho hicho kinazuia matumizi mabaya ya mchakato wa Mahakama.

“Waombaji waliahidi kuleta mashahidi 20 lakini walileta mashahidi 16. Nani aliwazuia kuleta mashahidi hao 20. Ukilalia haki yako huwezi kuja baadaye kulalamika,” alidai wakili Kalokola.

Kuhusu hoja ya kutajwa kwa Zitto mara nyingi alidai kuwa, katika shauri hilo wametajwa watu wengi wakiwamo askari, lakini hawajaitwa.

Pia, amedai kuwa Sheria ya Uchaguzi yenyewe inampa fursa mgombea kufungua shauri kulalamikia mambo yote yaliyojitokeza na akasisiza kuwa inampa nafasi anayeichangamkia haki na si anayeilalia.

Kuhusu vigezo vya kuongeza shahidi, wakili Kalokola alidai kuwa tangu shauri lifunguliwe ni muda wa miezi minane na kwamba haikubaliki kuongeza shahidi baada ya kuona namna mashahidi wanavyododoswa na kwamba hiyo itakuwa ni kuziba mapengo.

Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Singida Trading Store dhidi Kamishna Mkuu wa Malaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mashauri mbalimbali ya nje ya nchi, alidai kuwa zinazuia utaratibu wa kuleta shauri na kuvizia upande mwingine wanakujaje ili kuziba mapengo kwenye shauri wakati linaendelea

Vilevile wakili Kalokola alidai kuwa kesi za uchaguzi zina muda maalumu na kwamba kwa kutaka kuongeza mashahidi kwa kigezo cha kutajwa, kuna watu wengi waliotajwa nao itabidi waitwe.

“Kama haya yataruhusiwa sisi  upande wa walalamikiwa tutaathirika katika namna ya uendeshaji shauri hilo na mwenendo wa Mahakama pamoja na watu waliotajwa kwa vitendo vya utekaji na rushwa, kwa kuwa nao watalazimika kuitwa na hivyo shauri halitafika mwisho,” alisisitiza wakili Kalokola.

Akijibu hoja hizo wakili Seka alisisitiza kuwa, waombaji bado wana haki za kisheria na Kikatiba kuleta shahidi huyo ili wapate haki ya kusikilizwa kwa ukamilifu na kwamba Katiba inazuia kuminya haki hiyo kwa masharti ya kiufundi.

Kuhusu ya madai ya watu wengine kutajwa, watunga kanuni waliliona hilo katika kanuni ya 23 na kuweka hiyo haki.

Alidai kuwa, kwa maombi hayo hakuna suala la kufukia mashimo kwa kuwa, shahidi huyo akiitwa mawakili wa walalamikiwa pia watamhoji maswali ya dodoso.

Aliiomba Mahakama kama itaona si sawa walalamikaji kumuita basi yenyewe inaweza kumuita kwa sababu ni mtu muhimu katika shauri hilo.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Victoria Nongwa alisema kuwa kanuni  ya 21 inatumika kuomba kuongeza shahidi kabla ya mashauri kuanza kusikilizwa na kanuni ya 22 ndio inatumika baada ya mashahidi kuwa wameshahojiwa.

Alifafanua  kuwa kwanza shahidi inabidi awepo mahakamani na yeye mwenyewe aeleze sababu za maelezo yake kutowasilishwa mahakamani kwa wakati, lakini shahidi huyo hayupo na hajatoa sababu bali sababu zinatolewa na wakili.

Hivyo, alisema kuwa amekosa hoja ya msingi kwa waombaji na kwamba ingawa Mahakama ina utashi kuongeza mashahidi kwa kuzingatia busara zake na mazingira ya kesi na si kwa huruma.

Alisisitiza kuwa, baada ya usikilizwaji wa awali kufanyika na Mahakama ikapanga tarehe ya usikilizwaji kamili, waombaji waliwasilisha maombi ya kuongezewa muda kuwasilisha maelezo ya mashahidi na Mahakama kwa busara na kutokana na mazingira ikawakubalia.

“Waombaji walisema wangeleta mashahidi 20, lakini wakaamua kuleta maelezo ya mashahidi 16 ambao wamesikilizwa wote. Lakini, kama walitaka kuwaongeza, kanuni zinasema kuwa shahidi anapaswa kuwepo mahakamani na kueleza sababu,” alisema Jaji Nongwa.

 “Mashauri yanapaswa yafike mwisho. Ninaona kwamba haya ni matumizi mabaya ya mchakato wa Mahakama. Hivyo, maombi hayo ninayakataa.”

Kufuatia uamuzi huo wakili Seka alisema walalamikaji wanafunga kesi upande wao.

Jaji Nongwa aliwauliza mawakili pande zote iwapo wanahitaji fursa ya kuwasilisha hoja zao kama walalamikiwa wana kesi ya kujibu au la, ama wanaiachia mahakama iamue yenyewe.

Mawakili wa pande zote waliomba fursa hiyo huku wakipendekeza kuwasilisha hoja zao kwa njia ya mdomo.

Jaji Nongwa, hata hivyo aliamuru hoja hizo ziwasilishwe kwa njia ya maandishi na ingawa wakili Seka aliomba siku nne kujiandaa, walipewa siku tatu, akiwataka kuwasilisha hoja hizo kabla ya saa 6:00 usiku Julai 14 na akapanga kutoa uamuzi Julai 16, 2026 saa 4:00 asubuhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *