
Israel Katz, Waziri wa Vita wa utawala ghasibu wa Israel, amejibu matamshi ya hivi karibuni ya Donald Trump kuhusu kuondoka Israel katika ardhi ya Lebanon kwa kuyapinga vikali, na kusema Israel haitaomba idhini ya mtu yoyote katika kuendelea kusalia nchini Lebanon.
Maelewano yaliyofikiwa kati ya Iran na Marekani yanasisitiza ulazima wa kukomeshwa vita katika medani zote, ikiwa ni pamoja na Lebanon, na udharura wa kuondoka wanajeshi wa Kizayuni katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), kuna ukosoaji mkubwa kuhusiana na Marekani kuhusisha hali ya Lebanon na ya Iran. Wakosoaji wa Baraza la Mawaziri la Netanyahu, pamoja na baadhi ya mawaziri katika baraza hilo, wanaamini kwamba Donald Trump hana haki ya kuishinikiza Israel kuhusu Lebanon, hivyo wanasisitiza suala la kuendelea vita na kudumishwa uwepo wa kivamizi wa Israel kusini mwa Lebanon. Taarifa zilizotolewa na Katz pia zinaonyesha kwamba utawala wa Kizayuni hauna nia ya kuondoka Lebanon.
Malengo mawili makuu yanayofuatiliwa na utawala wa Kizayuni katika kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon ni kutaka kukata uhusiano mkubwa uliopo kati ya muqawama wa Lebanon na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na hivyo kubadilisha uwiano wa nguvu katika eneo kwa maslahi ya Tel Aviv, na pia kupanua wigo wa kijiografia wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Utawala wa Kizayuni unaamini kwamba hali ya sasa ya kikanda inatoa fursa nzuri ya kupanuliwa maeneo unayoyakalia kwa mabavu katika eneo. Hata hivyo, swali muhimu ni je, kuendelea vita na kukaliwa kwa mabavu Lebanon na utawala wa Kizayuni kutauletea matokeo gani utawala huo?
Moja ya matokeo ni kwamba, siasa za utawala wa Kizayuni za kuendeleza vita na kuikalia Lebanon kwa mabavu, zitadumisha machafuko na ghasia katika eneo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inachukulia kusitishwa mapigano na kuondoka majeshi ya Kizayuni kusini mwa Lebanon kuwa sharti muhimu la maelewano au makubaliano yoyote na Marekani. Mtazamo wa Wazayuni unaongeza uwezekano wa kushindwa kutekelezwa makubaliano yoyote muhimu na Marekani na hivyo kuanzisha tena mapigano haribifu na yenye madhara makubwa kwa eneo.
Matokeo mengine ni kwamba kuendelea kukaliwa kwa mabavu Lebanon kutaibua hisia na kukabiliwa vikali na Hizbullah, na hivyo kupelekea nchi hiyo kukumbwa na hali ya mivutano na ghasia zisizoisha. Wachambuzi wengi wa Israel pia wanaamini kuwa kuendelea kuwepo Israel nchini Lebanon hakutashindwa tu kurejesha utulivu kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, bali pia kutafungua njia ya majibu makali na makubwa zaidi kutoka kwa Mhimili wa Muqawama.
Matokeo mengine ni kwamba mtazamo wa utawala wa Kizayuni kuhusiana na Lebanon unahalalisha rasmi uvamizi wake. Kwa upande mmoja, utawala huo utaendeleza uvamizi, si nchini Lebanon pekee bali pia huko Syria na Gaza, ukiamini kuwa mfumo wa kimataifa hauna uwezo wa kukabiliana na uvamizi huo na kwamba Marekani, licha ya kupinga kidhahiri uvamizi huo, lakini kimsingi inaunga mkono ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Waarabu unaofanywa na utawala wa Kizayuni. Hoja ya mwisho ni kwamba sisitizo la utawala wa Kizayuni la kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon linabuni mfano hatari, kieneo na kimataifa, ambao unaweza kuzichochea tawala nyingine kukiuka mamlaka ya nchi nyingine kupitia vita na kukalia kwa mabavu ardhi zao. Hali hii inaweza kusababisha machafuko makubwa katika mfumo wa Kikanda na kimataifa katika eneo zima la Asia Magharibi.