Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotikisa mkoa wa kusini-magharibi mwa Pakistan wiki hii.

Siku ya Ijumaa, Msemaji wa Wizara hiyo, Esmaeil Baghaei, amelaani kwa ukali shambulio la kigaidi katika mji wa Khuzdar, katika mkoa wa Balochistan kusini-magharibi, ambalo limesababisha vifo na majeraha kwa raia wengi wa Pakistan.

Baghaei ametoa pole za dhati kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu kwa familia za wahanga, pamoja na kwa wananchi na serikali ya Pakistan.

Akisisitiza msimamo wa Iran wa kukataa aina zote za ugaidi na misimamo mikali ya kidini, Baghaei ameweka mkazo juu ya uhitaji wa kuimarisha ushirikiano na uratibu miongoni mwa nchi za kikanda ili kupambana na ugaidi kwa ufanisi na bila kukata. Amesisitiza kuwa hatua hiyo inapaswa kuhusisha kuwatambua, kuwatafuta, na kuwaadhibi wapangaji, wafadhili, na wasaidizi wa vitendo hivyo vya kigaidi.

Kwa mujibu wa jeshi la Pakistan, takriban watu 40 wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotokea mkoani Balochistan.

Siku ya Jumatatu, waasi walivamia kituo cha ulinzi kinacholinda mradi mkubwa wa bwawa la Mangi katika wilaya ya Ziarat, Balochistan, ambapo waliuwa maafisa tisa wa polisi na kuwateka nyara wengine 18. Waliotekwa nyara waliuawa baadaye.

Kisha, siku ya Jumatano, waasi hao walivamia gari lililokuwa likisafiri kwenye barabara kuu ya Balochistan na kuwaua wanajeshi 11.

Pakistan imekuwa ikipambana na uasi wa vikundi vya kigaidi vya wanaotaka kujitenga kwa miaka mingi katika mkoa wa Balochistan, ambao ndio mkoa mkubwa zaidi nchini humo lakini wenye watu wachache, ukipakana na nchi za Afghanistan na Iran.

Makundi ya wapiganaji kutoka kundi lililopigwa marufuku la Tehrik-e-Taliban Pakistan (TTP),ambalo ni tofauti na Taliban wa Afghanistan lakini lina uhusiano nao , pamoja na kundi lililopigwa marufuku la Balochistan Liberation Army, wamekuwa wakilenga vikosi vya serikali, miradi ya uwekezaji wa kigeni, na miundombinu katika eneo hilo lenye utajiri wa madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *