Unguja. Wafungwa nchini Zanzibar wanatarajiwa kupata fursa ya kujifunza taaluma za uhasibu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ujasiriamali na usimamizi wa fedha ili kuwawezesha kujiajiri au kuajirika baada ya kumaliza vifungo vyao.

Hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika maeneo 14 yanayolenga kuwajengea uwezo wafungwa na askari magereza.

Kupitia makubaliano hayo, wafungwa pamoja na watumishi wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar watanufaika na mafunzo mbalimbali yatakayowasaidia kupata ujuzi wa kitaaluma na wa vitendo kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika makao makuu ya Magereza Ziwani Zanzibar jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, alisema ushirikiano huo unalenga kuleta mabadiliko chanya kwa kuwapa wafungwa na askari maarifa yatakayowawezesha kujitegemea.

“Ushirikiano huu unalenga kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanafunzi na askari wa chuo hicho sambamba na kuandaa mitaala itakayowafaa, kufanya tafiti na ubunifu mbalimbali ili kuzalisha wataalamu wengi,” amesema.

Amesema miongoni mwa maeneo yatakayofanyiwa kazi ni utoaji wa programu za uhasibu, usimamizi wa fedha, ujasiriamali, Tehama, uthamini, masuala ya maktaba pamoja na tafiti na ubunifu.

Profesa Pallangyo amesema kupitia mafunzo hayo, wafungwa watakapomaliza vifungo vyao watakuwa na uwezo wa kutumia ujuzi walioupata kujiajiri, kutafuta ajira au kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunaboresha mafunzo yanayotolewa na kuleta manufaa kwa taifa. Tunategemea waliofungwa wakimaliza vifungo vyao warudi kwenye jamii wakiwa na uwezo wa kuajirika ikiwa itawezekana au kujiajiri na kuzalisha ajira,” amesema.

Amesema pia ushirikiano huo utasaidia kuwajengea uwezo katika utunzaji wa fedha na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za biashara, hatua itakayoongeza uwezo wa taasisi hizo kutoa huduma bora.

Amesisitiza kuwa TIA itatekeleza makubaliano hayo kwa uwajibikaji, weledi na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar, Omar Salum Mgaza, amesema makubaliano hayo yamefungua ukurasa mpya katika utoaji wa elimu kwa wafungwa na watumishi wa chuo hicho.

Amesema mafunzo hayo yatawalenga wafungwa na askari magereza kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya vifungo.

“Tutakuwa na mafunzo yanayolenga wafungwa waliopo gerezani pamoja na watumishi wa chuo cha mafunzo. Tunashukuru kwa fursa hii ya aina yake, awali hatukuwahi kupata mafunzo kama haya na tunaamini yataleta mabadiliko makubwa,” amesema.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kujenga mfumo wa kuwapatia wafungwa maarifa yatakayowawezesha kurejea katika jamii wakiwa na uwezo wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *