
UNAMKUMBUKA yule kipa Clause Kindoki aliyewahi kuitumikia Yanga? Jamaa amefariki jana Jumamosi Julai 11, 2026 kwenye ajali ya pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda ikiihusisha pia lori la mizigo.
Meneja wa zamani wa mshambuliaji, Fiston Mayele, Nestor Mutuale, amesema Kindoki amefariki saa chache baada ya kutoka uwanjani wakati timu aliyokuwa akiitumikia ya Ligi Daraja la Kwanza ya Bustras iliyopo jijini Lubumbashi nchini DR Congo iliposhinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Et Dauphin ya Goma.
Nestor ameeleza kwamba, Kindoki ambaye kabla ya umauti alikuwa kocha wa makipa wa Bustras, mara baada ya mchezo huo uliochezwa jijini Kinshasa, hakuondoka na basi la timu hiyo uwanjani hapo na baadaye kuamua kuchukua bodaboda ndipo baadaye akapata ajali hiyo, kisha lori kuja kumkanyaga.
“Nikweli Kindoki amefariki jana, kifo chake kimetusikitisha sana, tulikuwa naye uwanjani wakati timu yake ikicheza na ikishinda, alikuwa benchi na makocha wenzake,” amesema Nestor.
“Mchezo ulipokwisha akabaki pale uwanjani wakati basi la timu likiondoka, sijui hata kwanini alibaki, sasa baadaye akachukua moto (Bodaboda) na kuondoka.
“Akiwa njiani baada ya muda mfupi tukapigiwa simu kwamba amefariki, alipata ajali alipoanguka lori likaja likamkanyaga na kupoteza maisha. Alikuwa kijana mpole sana.
“Bado tunasubiri kujua taratibu za mazishi yake yatafanyika lini, klabu yake na familia watakaa na kutoa uamuzi.”
Kindoki aliitumikia Yanga msimu wa 2018-2019 wakati timu hiyo ikifundishwa na kocha Mwinyi Zahera, ambapo aliletwa sambamba na aliyekuwa mshambuliaji wa mabingwa hao, Heritier Makambo.