
Mfungwa mwanamke Mpalestina amesimulia uvamizi wa mara kwa mara, unyanyasaji wa kimwili na hali mbaya ya kizuizini inayowaathiri wanawake Wapalestina waliofungwa katika magereza ya Israel.
Ushahidi wa Shahd Muhammad Adi mwenye umri wa miaka 23 umewasilishwa kupitia wakili Hasan Abbadi na kuchapishwa jana Jumamosi na Kituo cha Habari cha Palestina.
Adi, mhitimu wa uuguzi kutoka mji wa Beit Ummar unaokaliwa kwa mabavu huko katika Ukingo wa Magharibi, amekuwa kizuizini katika magereza ya Israel tangu mwishoni mwa mwezi Machi. Amesema wafungwa wanawake wa Kipalestina wanasumbuliwa na unyanyasaji endelevu wakiwa mikononi mwa askari magereza wa Israel.
Kwa mujibu wa maelezo yake, walinzi wamekuwa wakivamia seli nyakati za Swala, kuwafunga macho na kuwashambulia wafungwa, na kuwalazimisha wanawake kuvua jilbabu zao huku wakiwa katika hali ya baridi kali.
Shahd Muhammad Adi amesema uvamizi mkubwa zaidi wa seli za magereza ulifanyika Mei 13, wakati askari magereza walipoingia katika sehemu ya wanawake huku wafungwa wakiswali nyakati za usiku.
Askari magereza waliripotiwa kurusha mabomu ya kushtua kwenye seli na kuwaingiza mbwa wa polisi kabla ya kuwaamuru wanawake hao kulala kifudifudi sakafuni. Adi amesema askari hao waliwaelekezea silaha wafungwa na kuwanyanyasa vibaya kwa maneno na kimwili.
Katika uvamizi huo pia askari magereza wa Israel walitwaa nakala za Qur’ani Tukufu kutoka kwenye vyumba vya wafungwa wa kike wa Kipalestina.
Ameongeza kuwa askari magereza wa Israel wamekuwa wakiwaingiza mbwa ndani ya seli za wafungwa wa Kipalestina mara kwa mara wakati wa uvamizi wa usiku, akitaja kitendo hicho kuwa ni jaribio la kuwatisha na kuwatia wahka wafungwa.
Ushuhuda wa Adi unakuja huku mashirika ya kutetea haki za wafungwa wa Palestina yakiripoti kuwa kuna ongezeko lisilo la kawaida la uvamizi unaolenga vyumba na seli za wanawake katika magereza ya Israel.
Chama cha Wafungwa wa Kipalestina kimesema uvamizi kadhaa uliohusisha vitengo maalumu vya askari magereza na mbwa wa polisi ulirekodiwa katika miezi mitatu iliyopita ya Julai. Shirika hilo pia limerekodi upekuzi wa kuaibisha wa kuvuliwa nguo watu, ukatili wa kimwili na aina nyingine za unyanyasaji dhidi ya wafungwa wanawake wa Kipalestina.