DODOMA: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amezitaka asasi zisizo ya kiserikali (NGOs) kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na serikali ili kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akifungua kikao kazi kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Baraza la Taifa la Mashirika asiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) leo (Julai 14, 2026) jijini Dodoma, Dk Gwajima amesisitiza kuwa mafanikio ya maendeleo yanapaswa kuonekana kupitia mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.
Moja ya ajenda kuu katika mkutano huo ni kujadili ushirikiano wa kimkakati kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, serikali imejipanga kubadilisha mfumo wa ushirikiano na NGOs kutoka kwenye utekelezaji wa miradi pekee na kuelekea kwenye ubia wa kimkakati wa Ttifa unaolenga kujenga Tanzania yenye ustawi na maendeleo endelevu.
“Tunataka kuhamisha mahusiano yetu kutoka kwenye ushirikiano wa miradi kwenda kwenye ubia wa kimkakati wa Taifa unaolenga kujenga Tanzania ya mwaka 2050,” amesema Dk Gwajima.
Ameeleza kuwa NGOs zina nafasi kubwa katika kujenga mtaji watu kupitia maeneo ya elimu, afya, lishe, uwezeshaji wa wanawake na vijana, ulinzi wa makundi maalum pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, ameyataka mashirika hayo kuhakikisha miradi inayotekelezwa nchini inaendana na vipaumbele vya Taifa na kuleta matokeo yanayopimika, ikiwemo kuongeza kipato cha wananchi, kupunguza umaskini, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Jasper Makalla, amesema sekta ya NGOs inaendelea kuwa mshirika muhimu wa serikali katika utoaji wa huduma za kijamii na kuchangia utekelezaji wa ajenda za maendeleo.
“Kadri tunavyoimarisha mazingira ya utendaji wa sekta, ndivyo tunavyozidi kuimarisha mchango wake kwa Taifa,” amesema Makalla.
Amebainisha kuwa kikao hicho ni sehemu ya mwendelezo wa majadiliano ya kimkakati kati ya Wizara na NaCoNGO yaliyolenga kuimarisha ushirikiano, uwazi na ufanisi wa sekta hiyo katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
