KLABU ya Yanga ishindwe yenyewe kukamilisha usajili wa mabeki wawili kutoka Mashujaa FC, Abdulnasir Assa ‘Gamal’ na Mohamed Mussa baada ya uongozi wa kikosi hicho kudai uko tayari kuwaachia ikiwa makubaliano ya pande zote yatafikiwa.

Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, inamuhitaji Gamal kwa ajili ya kuziba nafasi ya beki wa kulia, Israel Mwenda anayetajwa kutoendelea na kikosi hicho, huku kwa Mohamed Mussa ni chaguo la pili baada ya kumkosa nahodha wa TRA United, Nasri Kombo katika beki wa kati.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika amesema timu yoyote inayofika bei kwa mchezaji wa kikosi hicho wanafanya nao biashara, hivyo ikiwa Yanga inawahitaji wachezaji hao wanaruhusiwa kufanya pia mazungumzo.

YANG 01

“Sisi hatuna shida kwa sababu tunajua mpira ni biashara na lengo letu sio kumzuia mchezaji anapotaka kwenda timu yoyote kucheza, tunachotaka waje mezani tuzungumze vizuri na endapo tutafikia makubaliano tutaruhusu wawachukue,” amesema Tika.

Mwenyekiti huyo amesema wachezaji hao wote wawili bado wana mikataba ya miaka miwili kila mmoja ya kuendelea kuichezea Mashujaa, ingawa kuuzwa ni suala la mazungumzo na makubaliano yakifikiwa watawaachia ili wakaendelee kukuza safari yao ya uchezaji soka.

YANG 02
YANG 02

“Mchezaji anaposikia anatakiwa na timu hizi kubwa hata yeye mwenyewe huwa ni ngumu kumshawishi kuendelea kubakia, kama nilivyosema awali hatuna nia ya kumzuia mchezaji yeyote isipokuwa taratibu zifuatwe baina ya pande mbili,” amesema Tika.

Gamal alijiunga na Mashujaa msimu wa 2023-2024, akitokea Mlandege ya Zanzibar, huku kwa upande wa Mohamed Mussa anayecheza nafasi ya beki wa kati alitua katika timu hiyo Julai 23, 2025, baada ya kuachana na Kagera Sugar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *