Shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa (UN) limeonya kuwa Afrika Mashariki inaendelea kuwa kitovu cha janga kubwa la kibinadamu, huku watu wapatao milioni 48.5 wakihitaji misaada ya dharura mwaka huu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imebainisha kuwa mahitaji hayo makubwa ya kibinadamu yanasababishwa na migogoro, kuyahama makazi, majanga ya hali ya hewa, magonjwa, na uhaba wa chakula; huku tishio la kusambaa kwa virusi vya Ebola kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) likiongeza hatari zaidi kwa usalama wa kanda hiyo.

Katika ripoti yake iliyosambazwa Jumatano, OCHA imesisitiza: “Ingawa mlipuko wa Ebola bado umejikita zaidi nchini DRC, hatari ya kuenea katika kanda nzima bado ni kubwa.”

Kwa mujibu wa shirika hilo, hali ya ukosefu wa usalama wa chakula ilizidi kuwa mbaya katika robo ya pili ya mwaka, na kuacha watu milioni 40.5 wakikabiliwa na njaa kali, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 1.6 ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka 2025.

OCHA imebainisha kuwa ongezeko kubwa zaidi la uhaba wa chakula liliripotiwa nchini Sudan Kusini, Kenya, Sudan, na Tanzania.

Shirika hilo limebainisha kuwa athari za migogoro ya Mashariki ya Kati, ambao umesababishwa uingiliaji wa kibeberu wa Marekani na Israel, zinasababisha kupanda kwa gharama za mafuta, usafirishaji, na chakula, huku zikivuruga minyororo ya ugavi na kulemea uchumi ambao tayari ulikuwa dhaifu.

Aidha, majanga ya hali ya hewa yamesababisha takriban watu 13,000 kuyahama makazi yao nchini Burundi, huku idadi ya wakimbizi katika kanda hiyo ikipanda kutoka milioni 5.9 hadi milioni 6 hasa huko Sudan Kusini, Uganda, na Kenya.

Shirika hilo lilionya kuwa hatari za kiafya kwa umma katika kanda hiyo bado ni kubwa, huku visa vya kipindupindupindu katika robo ya pili vikiongezeka maradufu na kufikia 12,400, wakati visa 457 vya ugonjwa wa Mpox vikiripotiwa katika maeneo yaliyoathiriwa na watu kuyahama makazi yao pamoja na maeneo yanayokumbwa na mafuriko.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *