
Rasimu ya sheria ya kuvunjwa Bunge la utawala wa Kizayuni (Knesset) imepitishwa rasmi, hatua inayofungua njia ya kuitisha uchaguzi mpya wa mapema Israel.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuongezeka migogoro ya kisiasa ndani ya serikali ya muungano, huku tofauti kati ya vyama vinavyounda serikali zikizidi kuathiri uwezo wa serikali kuendelea kutawala.
Iwapo mchakato wa kisheria utakamilika, Knesset itavunjwa rasmi na uchaguzi mpya wa bunge utaitishwa kwa mujibu wa sheria za utawala wa Israel. Serikali ya sasa itaendelea na majukumu yake kama serikali ya mpito hadi serikali mpya itakapoundwa.
Mtandao wa habari wa i24 News wa utawala wa Kizayuni umetangaza kuwa Bunge la Israel (Knesset) limepitisha rasmi uamuzi wa kuvunjwa Buunge hilo, hatua inayohitimisha shughuli za muhula wake wa sasa na kufungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi wa mapema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wabunge wa Knesset walipitisha katika hatua ya mwisho muswada wa kulivunja bunge hilo, hivyo kumaliza rasmi shughuli za Bunge la 25 la utawala wa Kizayuni.
Nalo gazeti la Kiebrania la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa Bunge la 25 la utawala wa Kizayuni limeidhinisha kuvuunjwa shughuli za Bunge, huku uchaguzi wa mapema ukitarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja wakati utawala wa Kizayuni unakabiliwa na migogoro ya kisiasa na tofauti za ndani zilizochangia kuporomoka kwa muungano wa serikali na kuibua hitajio la kuitisha uchaguzi mpya.