INAELEZWA kwamba, ujio wa Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, unaifanya timu hiyo kuwa kwenye hatua za mwisho za kumalizana na nyota wawili wanaocheza soka Afrika Kusini, Justice Figuareido na Thulani Gumede.

Figuareido raia wa Eswatini anayecheza nafasi ya ushambuliaji na Gumede ambaye ni winga raia wa Afrika Kusini, ni machaguo ya Kocha Mngqithi kwani anafahamu vizuri uwezo wa nyota hao kutokana na walichokifanya katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini msimu wa 2025-2026.

Mngqithi aliyefundisha timu kadhaa Afrika Kusini ikiwemo Golden Arrows na Mamelodi Sundowns, inaelezwa baada ya kujiunga na Yanga amependekeza baadhi ya majina ya kuwasajili kipindi hiki cha dirisha kubwa.

Chanzo cha ndani kutoka Yanga, kimesema Figuareido aliyezaliwa Julai 28, 1998 (umri miaka 27) anatazamiwa kwenda kuimarisha eneo la mbele kwani licha ya kucheza mshambuliaji wa mwisho, pia ana uwezo wa kucheza kutokea pembeni winga zote.

Eneo hilo kwa sasa lipo wazi baada ya kuondoka kwa Prince Dube ambaye ndani ya kikosi cha Yanga, alikuwa akitumika kama mshambuliaji wa mwisho huku akiwa na uwezo wa kutokea pembeni.

“Yanga inaboresha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao ili kuendeleza kile tulichokifanya ndani ya misimu mitano mfululizo ambapo ni kuchukua ubingwa wa ligi,” kimesema chanzo hicho na kuongeza;

“Pia tunatarajia kuachana na wachezaji kama kiungo mkabaji Mohamed Damaro na beki Frank Assinki, ili wakapate changamoto mpya ya ushindani kwenye timu zingine na hilo ni jambo la kawaida.”

Baada ya Dube kurejea kwao Zimbabwe akisaini Hardrock FC, inailazimu Yanga kuingia sokoni kuziba nafasi hiyo kwani imebakiwa na mshambuliaji mmoja pekee aliye fiti ambaye ni Laurindo Aurélio ‘Depu’, huku Clement Mzize akiwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha.

Figuareido aliyemaliza msimu wa 2025-2026 akiitumikia Chippa United, amefanikiwa kuhusika na mabao saba katika mechi 26 alizocheza za Ligi Kuu ya Afrika Kusini ambapo amefunga mabao mawili na asisti tano.

Kwa upande wa Gumede kutoka Richards Bay aliyezaliwa Juni 15, 2001 (umri miaka 25), alimaliza msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini akihusika na mabao manne akicheza mechi 18, amefunga mabao mawili sawa na asisti.

Nyota huyu nafasi yake kubwa uwanjani ni winga wa kulia, lakini pia anaweza kucheza winga ya kushoto na kiungo mshambuliaji anayetokea kati.

Gumede kutakiwa kwake Yanga, ni kutokana na kuhitajika kuimarisha eneo la kushambulia pembeni baada ya Buba Jammeh kuonekana hajafiti kwenye mfumo tangu atue kikosini hapo ingawa wapo Maxi Nzengeli na Allan Okello wanaofanya vizuri.

Awali ilielezwa kwamba, Mngqithi baada ya kupata dili ndani ya Yanga, alifanya mawasiliano na winga Keletso Makgalwa kutoka Sekhukhune baada ya nyota huyo kuanza mazungumzo na Simba.

Hata hivyo, Keletso inaelezwa tayari amemalizana na Simba kwa mkataba wa miaka miwili, ndiyo maana Mngqithi amebadili gia na kumgeukia Gumede.

Wakati huohuo, kwa mujibu wa taarifa kutoka Eswatini, pande zinazohusika na dili la Figuareido walikutana Jumamosi iliyopita ya Julai 11, 2026, kujadili uwezekano wa kukamilisha uhamisho wa nyota hao.

Hata hivyo, licha ya taarifa hizo kuendelea kuenea, Figuareido anayecheza timu ya taifa ya Eswatini, amesema bado hajapata taarifa rasmi kuhusu mazungumzo hayo ya uhamisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *