WAKATI michuano ya Kombe la Dunia 2026 ikielekea ukingoni, wachezaji wa zamani wa Tanzania wametaka wadau wa soka hapa nchini kujifunza mambo mengi katika mechi hizo wakati Tanzania ikielekea kuwa mmoja wa wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027.
Akizungumza kwenye mdahalo maalum ulioandaliwa na Kampuni ya Bia ya Safari ambao ni moja wa wadhamini wa fainali za Kombe la Dunia 2026, Chambua amesema anaamini wachezaji mbalimbali wamejifunza mengi namna ya kucheza kwa kuitanguliza nchi yako.
Mkongwe huyo amesema wachezaji wana wajibu wa kucheza kwa uzalendo kwa kuipigania klabu au taifa lako wakati ukiwa uwanjani akitolea mfano namna ilichofanya Cape Verde na Iran.
“Zimekuwa fainali nzuri, ushindani ulikuwa mkubwa sana, nadhani kwa wachezaji wetu kuna mengi ya kujifunza, jambo la kwanza ni kucheza kwa uzalendo, hakuna ambaye alitarajia kuona ambacho Cape Verde ilifanya kwenye fainali hizi,” amesema Chambua.
“Tunaelekea kuandaa fainali za Mataifa Afrika mwakani tukiwa kama wenyeji, sasa kitu cha msingi ni wachezaji wetu kujua namna ya kucheza kwa kulipigania taifa lako lakini ndani yake watapata nafasi ya kuuza vipaji vyao.”
Wakati Chambua akiyasema hayo, winga wa zamani Mrisho Ngassa, ameongeza kuwa, anamini Tanzania ikiongozwa na serikali kupitia wizara ya michezo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakuwa limechukua mengi mazuri kuhusu mkiundo mbinu ya soka.
“Niliona waziri Makonda (Paul) alikuwa huko lakini pia Rais wa TFF, Karia (Wallace), sisi tumeangalia kwenye televisheni lakini tumevutiwa na miundombinu, viongozi wetu hawa walikuwa huko watakuwa wameyachukua mengi mazuri na kuja kujifunza katika viwanja vyetu nchini,” amesema Ngassa.
Mwaka 2027, Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, zitaandaa Fainali za AFCON, baada ya nchi hizo kutoka kuwa wenyeji wa CHAN 2025.