Dodoma. Ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Klarensi Usakazi (86), mkazi wa Kitongoji cha Mbisi, Tarafa ya Chipanga, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, aliyeamua mtalaka wa mtoto wake ‘mkamwana’ aitwaye Mary (20) baada ya wazazi wake kudai kutokuwa na uwezo wa kurudisha mahari.

Hata hivyo, Mary anakuwa mke wa nane kwa Usakazi, wakiwamo wengine watatu wa familia moja ‘pacha’, ambao anadai kufurahishwa na tabia ya ukoo wao hadi kufikia uamuzi wa kuwaoa.

Siyo jambo geni kwa mzee kuoa mke wa umri mdogo katika mila za wenyeji wa Dodoma, hali ambayo huitwa ‘Chikombipilo’ kwa maana ya binti atakayekuja kumtunza mumewe pindi atakaposhindwa kutimiza majukumu ya utafutaji.

Ilivyokuwa

Usakazi mwenye ukwasi wa mifugo karibu kila eneo la Tarafa ya Chipanga alimuoa Mary Chaina (20) kupitia ndoa halali ya kimila iliyofanyika Januari 25, 2024, baada ya kuolewa na Fredrick ambaye ni mtoto wake.

“Ni kweli alikuwa mke wa mtoto wangu Fed (Fredrick), lakini waliishi mwaka mmoja na wakaanza kusumbuana. Mimi nikaona bora nimuoe ili kijana akatafute mke mwingine anayempenda na alifanya hivyo. Nikalipa mahali,” amesema.

Katika mazungumzo yaliyofanyika nyumbani kwa mzee huyo, anakiri kwamba hakuwa akimjua Mary, lakini alimfahamu siku alipokwenda kumlipia mahali kwa lengo la kuolewa na mtoto wake Fredrick.

Hata hivyo, anafafanua kuwa kadri siku zilivyoenda wakati wakiishi wote, alibaini binti huyo hakuwa na tabia mbaya, isipokuwa kijana wake ndiye aliyekuwa tatizo katika ndoa yao.

“Sasa ningewezaje kumruhusu arudi kwao wakati nimelipa kwa wazazi wake ng’ombe watano, mbuzi 10 na fedha takribani Sh400,000? Nilipomuuliza binti kama yupo tayari kuolewa na mimi akakubali, basi nikamfanya kuwa mke wangu wa nane,” anasema Klarensi.

Kwa kauli yake anasema haoni tatizo ikiwa kijana wake ataamua kurudiana na mkewe, kwani atakuwa tayari kumruhusu, isipokuwa kwa sharti la kumdai mahali yake kwani alishamlipia na kumuoza mke mwingine.

“Huyu kwa sasa ni mke wangu halali, tunaishi kama mume na mke, anapika kwa zamu sawa na wenzake, nalala kwake kwa siku ambazo napanga mimi mwenyewe.

“Lakini kijana wangu akisema anamtaka tena mkewe, sitakuwa na ugomvi maana nimeshamchukua, lakini lazima alipe mahali yangu ili awe na wake wawili. Nililipa ng’ombe, mbuzi na pesa taslimu, lazima arudishe,” anasema.

Afikisha wake nane

Matukio ya mzee Usakazi hayaishi, kwani baada ya ndoa ya Mary ilimfanya kufikisha wake nane, wakiwamo watatu wa familia moja ambao ni pacha, aliodai kupenda ukoo wao kutokana na tabia zao.

Katika familia ya kikongwe huyo, hadi sasa ana watoto 48, wakiwamo wa kiume 30 na wa kike 18, huku akieleza kuwa siri ya kuoa ndugu wa familia moja ni kutafuta heshima na kuangalia historia nzuri ya ukoo kabla ya kufanya uamuzi.

Alipo Fredrick

Kwa sasa inadaiwa kuwa kijana Fredrick yupo mahabusu kwa tuhuma za kupanga njama za kumshambulia kaka yake kutokana na visa vya mifugo ya baba yao.

Taarifa ambazo si rasmi zinadai kuwa kukamatwa kwa kijana huyo kunamhusisha baba yake, kwamba alishinikiza akamatwe baada ya kuona dalili za kutaka kumchukua mke wake, Mary.

“Hizo taarifa si za kweli. Mimi sijampeleka rumande kwa sababu hata mke wake yupo hapa nyumbani, matumizi nalipia mimi. Nimempa fedha akajenga nyumba ya vyumba viwili kwenye eneo langu.

“Yule ni mwanangu, hivyo siwezi kumfunga, isipokuwa alipanga njama za kumvamia kaka yake, wakampiga mapanga, ndiyo akakamatwa na sheria kuchukua mkondo wake,” anasema Klarensi.

Mary afunguka

Kwa aibu na hofu ya kutokumtazama mtu usoni, Mary anasema: “Nilikubali kuolewa na huyu mzee ili anitunze nami nipate mji wangu. Huyo mtoto wake alikuwa ananitesa, lakini huyu mume wangu wa sasa hana shida,” anasema Mary.

Alipoulizwa kuhusu umri wake kuwa mdogo, kwa kujiamini anasema kuwa amefikisha miaka 20, hivyo anastahili kupata mume na kwa sasa aliyemwona ni huyo mzee, akiamini ndiyo chaguo lake na ndoto yake ya maisha.

“Fredrick aliamua kunikataa mwenyewe. Kama asingefanya hivyo, mimi ningeendelea kuwa naye maana nilimpenda sana, lakini kwa sasa ni kama rafiki tu, tunaishi bila tatizo,” anasema Mary.

Kuhusu kama Fredrick angetaka kumrudisha, Mary anaeleza kuwa haitakuwa tatizo, isipokuwa azungumze na baba yake wakubaliane ili isitokee mtafaruku, na kwamba yuko tayari kurudiana naye.

Kwa upande wake, Winifrida Chilongozi, mmoja wa wake wa Usakazi, anakiri kuwa Mary ni mke mwenza wake na wanaachiana zamu ya kumhudumia mume wao, ingawa awali alikuwa mkwe.

Baba wa Mary

Chaina Masingwe, ambaye ni baba mzazi wa Mary, amesema suala la mahali halikuwa tatizo kwake, isipokuwa aliona binti mwenyewe amekubali kuishi na mzee huyo na kumpa baraka zote.

“Mary ni mwanangu, alizaliwa mwaka 2006. Kwenye elimu aliishia darasa la tatu. Yule mzee hakuwa mumewe bali kijana wake. Sasa kwenye ugomvi wao ndiyo huyo mzee Usakazi akasema anamuoa yeye.

“Nilipomuuliza binti yangu kama anaridhia kuolewa na mzee huyo, alisema amekubali. Kama wewe ungefanyaje wakati huo tayari nimekula mahali ya watu?” anasema Masingwe.

Wadau wafunguka

Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Mustafa Rajab, anasema jambo hilo halikubaliki, tena linatoa picha mbaya ambayo inapaswa kupigwa vita kwa namna zote.

Alhaji Mustafa, ambaye ni kiongozi wa Umoja wa Viongozi wa Dini Mkoa wa Dodoma, anasema kitendo hicho kinaonyesha ndani ya familia hiyo kumekosekana elimu na hivyo kuna haja ya kuwepo juhudi za kuikomboa kielimu.

“Haikubaliki, lazima kitendo hicho kipingwe kwa nguvu zote. Haiwezekani kwani hakileti picha nzuri. Huenda familia hiyo imekosa elimu, hivyo tuwafikie ili kuwanusuru,” amesema shekhe huyo.

Mwanaharakati wa haki za jinsia, Janeth Makini, amesema hizo ni mila kandamizi na kwamba umaskini wa baba mzazi wa binti umetumika kama fimbo ya kumuumiza mtoto huyo.

“Huo ni udhalilishaji mkubwa, ni utumwa wa ngono. Mke amegeuzwa kuwa ngoma kila mtu anapiga. Si sawa kabisa na, nionavyo mimi, huyo binti bado yuko utumwani. Anahitaji sauti za watu ili akombolewe kwenye dimbwi hilo,” anasema Janeth.

Kwa upande wake, Chifu Lazaro Chihoma anasema katika mila za Wagogo hakuna utamaduni kama huo, badala yake anaufananisha na laana inayozunguka kwenye ukoo.

“Sasa ukikuta mtu anafanya matendo hayo, unamtofautishaje na yule anayeweza kuoa binti yake? Kwenye mila za Wagogo huyo anapaswa kuitwa na kuonywa, alipe faini kwanza, kisha amwache binti huyo kuliko kuoa mke wa mtoto wake,” amesema Chifu Chihoma.

Mmoja wa viongozi wa kijiji hicho ambaye hakupenda kuandikwa jina, anasema maisha ya mzee huyo huwa ni ya kujitenga huku akijivunia wingi wa mifugo yake, ingawa baadhi ya vijana wake ambao ni watu wazima wamekuwa washirika wa maendeleo kwa karibu.

Anasema mzee huyo hupenda kufanya maamuzi yake mwenyewe bila ushirikishwaji, lakini wengi hupata hofu ya kuingia kwenye boma lake lililozungukwa na nyumba nyingi, ikiwamo mifugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *