
Rais Donald Trump wa Marekani ameachana na mpango wake wa kutoza ushuru wa asilimia 20 kwenye Lango Bahari la Hormuz.
Trump ambaye awali alidai kwamba Marekani ina nia ya kuwa “mlinzi wa Lango-Bahari la Hormuz” na kusema atatoza ushuru wa asilimia 20 kwenye njia hii ya maji ambayo hana mamlaka nayo, hatimaye ameachana na ndoto hiyo isiyothibiti.
Trump, ambaye anajulikana kwa kuwasilisha mipango kama hiyo ya kiigizaji isiyo na msingi wowote wa kimantiki, alidai kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba: “Kwa mujibu wa mazungumzo mazuri sana na viongozi wa Mashariki ya Kati, nimeamua kubadilisha ushuru wa asilimia 20 na mikataba ya biashara na uwekezaji ambayo mataifa mbalimbali ya Ghuba ya Uajemi yatafanya nchini Marekani.” Kufuatia kauli hiyo, Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ameandika kwenye mtandao wa X: “Rais wa Marekani amesema ukweli kabisa. Yeyote anayedhamini usalama na upitaji salama wa meli za biashara katika Lango la Hormuz anastahiki kulipwa fidia kwa huduma hiyo.” Amesisitiza: “Iran imekuwa ikilinda usalama katika Lango la Hormuz siku zote na itaendelea kufanya hivyo milele. Bila shaka, asilimia 20 ni kiwango cha juu sana; Sisi tutakuwa na insafu na kutoza ada nafuu zaidi!”
Inaonekana kuwa hatua ya Trump kurejea nyuma ghafla inatokana na mchanganyiko wa mashinikizo ya ndani, upinzani kutoka kwa washirika wa kikanda, changamoto za kisheria na tathmini za kimkakati. Sababu kuu iliyompelekea kubadili msimamo ni mashinikizo ya pamoja kutoka kwa washirika wake wa Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Ripoti zinaonyesha kuwa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC)—zikiwemo Saudi Arabia, UAE, Qatar, Kuwait, na Bahrain, zilichukua msimamo wa pamoja wa kupinga mpango huo. Hoja yao kuu ilikuwa kwamba hatua ya Marekani ya kutoza ada kama hizo inaweza kutoa mwanya kwa mataifa mengine kuchukua hatua kama hiyo katika njia nyingine za maji duniani.
Sababu nyingine ni kukosekana msingi wa kisheria wa kuunga mkono mpango huo wa Trump na kutooana kwake na sheria za kimataifa. Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) limetangaza kuwa kutoza ada za lazima kwa meli zinazopita katika njia za maji za kimataifa hakuna msingi wowote wa kisheria. Cha kuzingatiwa ni kwamba, Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, awali alikuwa amesisitiza kuwa “hakuna nchi yoyote inayoruhusiwa kuweka ushuru kwenye njia za maji za kimataifa.”
Sababu ya tatu inahusiana na gharama kubwa za kiuchumi na taathira za kisiasa za ndani zinazotokana na mpango huo wa Trump. Wataalamu wa uchumi wameonya kuwa kuweka ushuru wa asilimia 20 kwenye shehena zinazopita katika Lango-Bahari la Hormuz kunaweza kupelekea kupanda kwa bei za bidhaa duniani na hatimaye kuongeza mzigo kwa watumiaji bidhaa wa Marekani. Kwa kuzingatia uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani uliopangwa kufanyika Novemba 2026, kupanda kwa bei ya bidhaa kunaweza kuathiri vibaya sana uungaji mkono kwa Trump na Chama cha Republican. Tafiti za maoni zinaonyesha kuwa vita dhidi ya Iran vinapingwa na umma wa Marekani, huku kupanda kwa bei ya mafuta kukishusha umaarufu wa Trump hadi kiwango cha chini kabisa tangu aingie madarakani.
Sababu ya nne ni kutokuwepo mkakati madhubuti na mshikamano katika utendaji wa Trump kuhusu uchukuaji maamuzi. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaelezea maamuzi ya ghafla ya Trump kama ishara ya “kutokuwa na mwelekeo wa kimkakati” na “mkanganyiko” kuhusiana na Iran. Wanaamini kwamba, Trump anafuatilia malengo mawili yanayokinzana kwa wakati mmoja. Kwa upande mmoja, anataka kufikia makubaliano na Iran, huku kwa upande wa pili, akitishia kuharibu ustaarabu wa Iran. Kufanya maamuzi ya ghafla, bila kushauriana na washirika, ni sifa kuu ya tabia ya Trump, ambayo imedhihiri wazi katika mpango huu pia. Sababu ya tano ni kupitishwa kwa mkakati mbadala. Kwa uchache kwa mtazamo wa nje, badala ya kutoza ada za moja kwa moja, Trump amejikita katika mikataba ya kibiashara na mataifa ya Ghuba ya Uajemi pamoja na kuvutia uwekezaji wao nchini Marekani. Mabadiliko haya ya mbinu yalitangazwa sambamba na kuimarishwa kwa mzingiro wa majini dhidi ya Iran na vitisho vya kushambulia miundombinu ya Iran. Hivyo, kwa mtazamo wake, Marekani inaepuka gharama za kisiasa na kiuchumi zinazotokana na kutoza ada za moja kwa moja kwa meli, huku ikiendelea kudumisha “mashinikizo ya kiwango cha juu” dhidi ya Iran.
Kwa ujumla, hatua ya Trump ya kuachana na mpango wa kutoza ada ya asilimia 20 kwa usafirishaji wa meli kupitia Lango-Bahari la Hormuz inaonekana kama ishara nyingine ya kufeli kwa hatua za upande mmoja na zisizo halali zinazochukuliwa na Marekani ndani ya mfumo wa kimataifa.