
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeharibu kituo cha rada cha jeshi la Marekani katika Kituo cha Anga cha Ali Al Salem na kushambulia mkusanyiko wa wanajeshi wa nchi hiyo katika Kambi ya Arifjan huko Kuwait katika wimbi la 18 la Operesheni Nasr 2.
Katika taarifa iliyotolewa mapema leo Jumamosi, IRGC imesema kikosi chake cha nchi kavu kimelenga “eneo la mkusanyiko wa wanajeshi vamizi wa Marekani” katika kituo cha msaada na zana za jeshi la nchi hiyo huko Camp Arifjan, na kusisitiza kuwa maafisa kadhaa wa jeshi hilo wameuawa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa shambulio la ndege zisizo na rubani za IRGC limeharibu mfumo wa rada katika Kituo cha Anga cha Ali Al Salem.
Taarifa hiyo pia imesema vikosi vya jeshi la Iran vimeshambulia mabanda ya matengenezo ya ndege za kivita na maficho ya ndege zisizo na rubani, na kuongeza kwamba “shughuli za kulipiza kisasi za Jeshi la Nchi Kavu zitaendelea.”
Ikieleza kwamba vikosi vya jeshi la Marekani vimebadilisha mbinu kutoka mapigano ya moja kwa moja ya kijeshi hadi kwenye mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia, IRGC imeongeza kuwa Marekani inashambulia “hospitali, madaraja, reli, viwanja vya ndege, bandari, vituo vya mawasiliano na raia” katika jaribio la kuficha kushindwa kwake katika uwanja wa vita.
Taarifa hiyo imesema kwamba, kwa sababu “hakuna chombo cha kimataifa cha kuzuia ukatili wa jeshi la Marekani,” Iran haina chaguo ila kujibu kwa njia hiyo hiyo, ikinukuu kanuni ya Qur’ani inayosema: “Yeyote atakayekutendeeni ubaya, mtendeeni kwa kipimo kile kile alichokutendeeni ubaya.”
IRGC pia imezionya nchi zinazowahifadhi wanajeshi wa Marekani ambazo zimeruhusu ardhi zao kutumika kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Iran ikisema zinapaswa “kuwa tayari kwa majibu sawa” na kuzihimiza kuchukua hatua za ulinzi wa raia ili kuwalinda raia na kuwaweka mbali na shabaha za kijeshi.
Taarifa hiyo imesema Iran “kwa sasa” imeelekeza majibu yake kwenye shabaha za kijeshi tu “ili kumpa adui fursa ya kubadilisha mbinu yake haramu.”
Katika taarifa nyingine, IRGC imesema jeshi lake la wanamaji limefanya mashambulizi ya pamoja ya ndege zisizo na rubani na makombora kujibu mashambulizi ya Marekani usiku kuamkia leo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikosi vya jeshi la Iran vimeshambulia maghala ya mafuta ya meli za Marekani katika Bandari ya Al Ahmadi huko Kuwait, maegesho ya ndege za kijeshi za Marekani katika Kituo cha Anga cha Sheikh Isa huko Bahrain, na kituo cha data cha ujasusi huko Bahrain kilichotambuliwa kama Batelco.
IRGC pia imesema vikosi vyake vya majini vimeharibu kituo cha mawasiliano cha Marekani huko Kuwait.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa mashambulizi hayo yamefanyika huku Jeshi la Wanamaji la IRGC likiendelea “kudhibiti kikamilifu Lango-Bahari la Hormuz.”