ALIYEKUWA kocha wa Mamelodi Sundowns, Manqoba Mngqithi, mwenye umri wa miaka 55, ambaye hivi karibuni alikamilisha dili la kuwanoa mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC, anaripotiwa kuwa benchi lake la ufundi litakuwa na watu wengi wenye majina makubwa kutoka Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) akiwemo kiungo wa zamani wa Crystal Palace, Kagisho Dikgacoi na Mnigeria, Greg Etafia.

Baada ya kutambulishwa rasmi kuwa kocha mkuu wa Yanga, Mngqithi anaelezwa kuanza kuangalia soko la PSL ili kuimarisha benchi lake la ufundi.

Kocha huyo wa zamani wa Golden Arrows, anayejulikana kwa uwezo mkubwa wa kiufundi na mafanikio aliyoyapata akiwa Mamelodi Sundowns, analenga kuendeleza mafanikio hayo Afrika Mashariki kwa kuambatana na wataalamu kutoka Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa iDiski Times, Mngqithi yuko mbioni kuunganishwa na kundi la wataalamu wenye heshima kubwa kutoka PSL.

CRY 01

Miongoni mwao ni aliyekuwa kiungo wa timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) na klabu ya Crystal Palace, Kagisho Dikgacoi, ambaye anatarajiwa kuwa kocha msaidizi pamoja na Simo Dladla, huku Yanga ikilenga kuendelea kutawala mashindano ya ndani na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

Dikgacoi aliachwa na Golden Arrows baada ya Mngqithi kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa 2025-2026.

Kwa mujibu wa vyanzo vya Soccer Laduma, Dikgacoi alisafiri kwenda Tanzania usiku wa Alhamisi, Julai 16, 2026.

“Alionekana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo akiwa pamoja na wachezaji wa Mamelodi Sundowns ambao nao walikuwa wakisafiri kuelekea Austria. Aliwaambia kuwa yeye anaelekea Tanzania,” kimesema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina.

Soccer Laduma imebaini kuwa, Dikgacoi ataungana na benchi la ufundi la Mngqithi ndani ya Yanga, hivyo wawili hao wataanza kufanya kazi pamoja kwa mara nyingine, safari hii katika mradi wa kuijenga klabu hiyo ya Tanzania na Afrika Mashariki.

Kwa upande wa Dladla, Julai 6, 2026, aliaga ndani ya AmaZulu FC akisema: “Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa AmaZulu FC, Rais wa klabu, timu ya ufundi, timu ya matibabu, wachezaji, wafanyakazi wa usaidizi, na wafuasi waaminifu kwa kunipa fursa ya kuchangia timu msimu huu.

“Tulimaliza katika nafasi ya nne na kufanikiwa kufikia malengo yote yaliyowekwa kwa ajili ya kampeni. Imekuwa heshima na fursa kuwa sehemu ya safari hii.

“Kwa kuwa mkataba wangu umefikia mwisho, nataka kuwashukuru kila mtu katika klabu kwa msaada wao, taaluma, na imani yao kwangu. Kumbukumbu na uzoefu vitabaki nami kila wakati.

CRY 02

“Asante tena kwa familia nzima ya AmaZulu. Natamani klabu iendelee kufanikiwa katika siku zijazo.”

Hata hivyo, harakati za kuimarisha benchi la ufundi hazitaishia kwa makocha wasaidizi pekee, kwani Mngqithi pia anaripotiwa kumjumuisha aliyekuwa kipa wa kimataifa wa Nigeria, Greg Etafia, kuwa kocha wa makipa.

Etafia, ambaye ana uzoefu mkubwa ndani ya PSL, anaonekana kuwa nyongeza muhimu kwa Yanga wanapojiandaa na msimu wenye ratiba ngumu ya mashindano.

Katika hatua inayoonyesha matumizi ya mbinu za kisasa katika soka, benchi hilo pia linatarajiwa kumuhusisha mchambuzi wa utendaji (Performance Analyst) wa Bafana Bafana, Yardaan Valodia.

Mchanganyiko huo wa uzoefu mkubwa wa wachezaji wa zamani pamoja na utaalamu wa kisasa wa uchambuzi unaonyesha kuwa Mngqithi anajenga benchi la ufundi lenye uwezo wa kukabiliana na presha ya kuiongoza moja ya klabu kubwa zaidi barani Afrika.

Ingawa Yanga imekuwa ikipeperusha vyema bendera katika Ligi Kuu ya NBC kwa kutwaa ubingwa katika misimu mitano iliyopita, lengo kuu la benchi jipya la ufundi litakuwa kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).

Mngqithi anafahamu vyema kinachohitajika kutwaa taji hilo, kwani alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Pitso Mosimane lililoiongoza Mamelodi Sundowns kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2016.

Rekodi ya Mngqithi pia inazungumza yenyewe. Akiwa kocha wa Golden Arrows aliiongoza timu hiyo kutwaa taji lake pekee kubwa la ndani mwaka 2009 baada ya kuichapa Ajax Cape Town mabao 6-1 katika fainali ya MTN8.

Historia hiyo ya mafanikio, pamoja na uzoefu alioupata kwa miaka mingi ndani ya utamaduni wa ushindi wa Mamelodi Sundowns, inamfanya Mngqithi kuonekana kuwa chaguo sahihi la kuipeleka Yanga katika kiwango cha juu zaidi barani Afrika.

Hivi karibuni, Mwanaspoti iliripoti kwamba, Mngqithi amekubaliana na mabosi wa klabu hiyo kuwa ataendelea kufanya kazi na Abdihamid Moallin ambaye alikuwa kama kaimu kocha mkuu akiwapa ubingwa timu hiyo baada ya kuondoka kwa Pedro. Pia mtaalam wa kutunza taarifa za ubora na viwango wa wachezaji wa timu (Perfomance analyst) atasalia Msauzi, Thulani Thekiso ambaye anaungana na anayekuja ambaye atafanya wataalam hao kuwa wawili kwenye kikosi hicho.

Aidha, kocha huyo amembakisha kocha wa mazoezi ya viungo, Chyna Mokaila raia wa Botswana akiwathibitishia mabosi wa klabu hiyo kuwa anamjua jamaa huyo na kazi yake ni nzuri.

Awali upepo haukuwa vizuri kwa Mokaila wakati Yanga ikiwa haifanyi vizuri chini ya Pedro msimu uliopita, ilibaki kidogo atolewe kabla ya uamuzi huo kusitishwa na sasa kocha mpya amembakisha zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *