Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kujenga uchumi unaotegemea maarifa, sayansi na teknolojia, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeanza mkakati wa kuwawezesha wabunifu vijana kwa kuwapatia mitaji ya kuendeleza bunifu zao, hatua inayotarajiwa kuzifanya zigeuke biashara na suluhisho la changamoto za jamii.

Hatua hiyo inalenga kuziba pengo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiwakabili wabunifu wengi nchini, ambapo mawazo na teknolojia wanazobuni huishia katika maonyesho bila kufikia hatua ya kuzalishwa kwa wingi au kuingia sokoni.

Akizungumza baada ya kukagua mabanda ya maonyesho ya ubunifu wa wanafunzi, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa wa Costech, Samson Mwera amesema wabunifu na wataalamu vijana watakaokidhi vigezo wataunganishwa na fursa za mitaji ili kuendeleza miradi yao.

Amesema Tanzania inaendelea kujenga kizazi chenye uwezo wa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo, jambo linalodhihirishwa na kazi zinazowasilishwa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Lengo letu ni kuhakikisha bunifu hizi haziishii darasani. Tunataka ziwe bidhaa na huduma zinazotatua changamoto za jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi. Ndiyo maana tumeanza mkakati wa kuwawezesha wabunifu watakaokidhi vigezo kwa kuwapatia mitaji ya kuziendeleza,” amesema Mwera.

Katika maonyesho hayo, wanafunzi walionyesha bunifu mbalimbali za kiteknolojia zikiwemo mfumo wa kupunguza msongamano wa magari katika makutano ya barabara kwa kutumia teknolojia, mfumo wa Smart Parking unaowaelekeza madereva maeneo ya maegesho kupitia mifumo ya mwanga, pamoja na matumizi ya teknolojia ya uchapishaji wa pande tatu (3D Printing) kutengeneza bidhaa mbalimbali, ikiwemo mfano wa Kombe la Dunia.

Mwera amesema jambo linalotia moyo ni kwamba wanafunzi hao wameanza kujifunza programu za kompyuta tangu ngazi za awali za elimu, hatua inayowajengea msingi wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaolengwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema mwelekeo huo pia unaendana na sera ya elimu inayosisitiza mafunzo ya amali, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Community, Baraka Yusuf Jacobo Magiri, amesema taasisi hiyo imeamua kushirikiana na Serikali kuimarisha elimu ya teknolojia kuanzia ngazi ya shule kwa kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi.

Amesema ni wakati wa mfumo wa elimu kuendana na kasi ya maendeleo ya dunia kwa kuimarisha ufundishaji wa masomo ya coding, robotics na Akili Unde.

“Tunataka walimu waweze kutumia teknolojia darasani badala ya kutegemea ubao na chaki pekee. Hii itawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kukuza uwezo wao wa ubunifu,” amesema.

Pia ameitaka Serikali kuendelea kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya kufundishia, ikiwemo mbao za kuandikia na zana nyingine za kidijitali ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Naye mwalimu wa Shule ya Msingi Tegeta A ya jijini Dar es Salaam, Pendo Mwandiga, amesema maonyesho hayo yameongeza hamasa kwa wanafunzi kwa kuwapa nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao na kuonyesha kuwa ubunifu unaweza kutumika kutatua changamoto za kila siku.

“Wanafunzi wanapokutana na kuona bunifu za wenzao wanapata motisha wa kufikiria zaidi, kuibua mawazo mapya na kuamini kuwa wanaweza kutumia teknolojia kubadilisha maisha yao na ya jamii,” amesema.

Kwa mujibu wa Costech, mpango wa kuwapatia mitaji wabunifu vijana ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha bunifu zinazozalishwa nchini zinageuzwa bidhaa na huduma zenye thamani ya kiuchumi, hivyo kuongeza ajira, kukuza viwanda vinavyotegemea teknolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *