Singida Black Stars inaendelea kushusha vyuma vipya kimya kimya kwa ajili ya kukisuka kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027 na kwa sasa imefikia makubaliano ya kumsajili aliyekuwa winga wa Simba raia wa Ivory Coast, Aubin Kramo.

Kramo aliyejiunga na Simba Agosti 1, 2023, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, alishindwa kuwika na kikosi hicho cha Msimbazi kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, jambo lililosababisha kuachwa Agosti 22, 2024.

Nyota huyo aliyewika na timu mbalimbali,  amejiunga na Singida baada ya kuachana na Ittihad Gharyan SC ya Libya.

Hata hivyo, taarifa kutoka uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti licha ya baadhi ya wachezaji wengi wa kigeni kusajiliwa, ila hatima ya mwisho ya kukamilisha uhamisho wao utategemea na kuridhishwa na benchi lao la ufundi.

KIU 01

“Wachezaji wengi tuliowaleta tutakamilisha usajili wao ikiwa benchi la ufundi litaridhika na viwango vyao, tutatumia hii Michuano ya Kombe la Kagame ili kuwaangalia fitinesi zao kabla ya kufanya uamuzi huo wa mwisho,” kilisema chanzo hicho.

Nyota wengine watakaoangaliwa kabla ya kusajiliwa pia moja kwa moja ni kiungo Dramane Kambou raia wa Burkina Faso anayetoka FC Saint-Eloi Lupopo ya DR Congo na kiungo mshambuliaji raia wa Austria, Marcel Canadi ambaye kwa sasa ni mchezaji huru.

Canadi aliyewahi kuichezea Klabu ya Borussia Monchengladbach II ya Ujerumani, kwa sasa yupo huru baada ya mchezaji huyo kuachana na Enosis Neon Paralimni FC kutokea Cyprus aliyojiunga nayo Januari 1, 2025, akitokea Lexington SC ya Marekani.

KIU 02

Wachezaji wa kigeni wenye uhakika wa kusajiliwa moja kwa moja ni mawinga, Exauce Sagesse Nzaou anayetokea AS Otoho d’Oyo ya Congo Brazzaville na Mnigeria Henry David aliyeifungia Fountain Gate mabao manne ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *