
UONGOZI wa Geita Gold umefungua mazungumzo ya kuipata saini ya kipa wa TS Galaxy ya Afrika Kusini raia wa Nigeria, Kayode Bankole Iyanu kwa lengo la kuimarisha kikosi hicho msimu ujao wa 2026-2027, wa mashindano mbalimbali hasa ya Ligi Kuu.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti Kayode ni miongoni mwa makipa wa kigeni wanaopigiwa hesabu za kujiunga na kikosi hicho, ambacho ndio mabingwa pia wa Ligi ya Championship kwa msimu uliopita wa 2025-2026.
“Mazungumzo yamefikia hatua nzuri na kilichobakia ni mambo machache ambayo kuanzia wiki hii inayoanza leo Jumatatu ya Julai 20, 2026, tunaweza kukamilisha, suala la maslahi sio tatizo na tunaamini tutakubaliana,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema uzoefu wa mchezaji huyo ni chachu ya kuongeza ushindani msimu ujao, ambapo kwa sasa mabosi wa timu hiyo wamejipanga kuongeza wachezaji wengi watakaoleta morali ya kukipambania kikosi hicho katika mashindano mbalimbali.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zubery Katwila aliyeipandisha timu hiyo daraja kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara, amesema baada ya msimu wa 2025-2026, kumalizika alitoa mapendekezo yake yote kwa ajili ya kufanyiwa kazi haraka.
“Tayari kuna wachezaji tunaendelea kukamilisha baadhi ya taratibu zote muhimu kisha baada ya hapo uongozi utawatangaza rasmi kwa ajili ya kuitumikia Geita Gold msimu ujao, hivyo, kwa sasa naomba tuendelee kuvuta subra,” amesema Katwila.
Kayode aliyezaliwa Oktoba 16, 2002, ni kipa mzoefu aliyecheza klabu mbalimbali za Shooting Stars FC kuanzia mwaka 2019 hadi 2020, kisha Remo Stars FC 2020–2025 zote za kwao Nigeria na mwaka 2025, alijiunga na TS Galaxy FC ya Afrika Kusini.