YANGA imeonyesha kuwa haitanii na sasa inadaiwa kuwa imeshamshusha mshambuliaji, Husseni Mihambo Dar na kumpa mkataba wa miaka minne akitokea Mashujaa FC, usajili unaotajwa kuwa miongoni mwa uliogharimu fedha nyingi kwa mchezaji chipukizi dirisha hili.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara imeendelea kuboresha kikosi chake kwa kuhakikisha inashusha wachezaji wengi bora ili iweze kufanya vizuri kuanzia kwenye Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la CRDB msimu ujao.
Timu hiyo imeendelea kuwaamini wachezaji wanaochipukia baada ya juzi kumtambulisha Issa Abushiri ‘Chuga Boy’ kutoka Fountain Gate ikiendelea kuonyesha makali yake kwenye usajili.
Mihambo anajiunga na mabingwa hao watetezi kukiwa na ushi ndani mkubwa wa nafasi ndani ya kikosi hicho kwenye nafasi ambayo tayari ina majina makubwa akiwemo Clement Mzize, Laurindo Depu, Emmanuel Mwanengo na Edmund John ambao hawapata nafasi ya kucheza mara kwa mara, hata hivyo anatakiwa kupambana kuhakikisha anamshawishi kocha mpya wa timu hiyo Manqoba Mngqithi.
Anajiunga na Yanga akiwa anajua wazi kuwa nafasi anayocheza sio rahisi kutokana na waliopo ambao tayari wameshajitengenezea namba kikosini. Kabla ya kutua Jangwani, Mihambo aliwahi kucheza soka la vijana katika klabu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini, na kufanya majaribio nchini Dubai kwa zaidi ya mwaka mmoja ingawa hakufaulu.
Akiwa na Mashujaa FC msimu uliopita, mshambuliaji huyo hakupata nafasi ya kucheza kwenye mechi nyingi kutokana na ushindani wa kikosi, alifanikiwa kufunga bao moja.
Chanzo kiliambia Mwanaspoti kuwa tayari mshambuliaji huyo amemalizana kila kitu na wananchi hao kilichosalia kutambulishwa tu.
“Juzi walikuwa na maandalizi ya kupiga picha kwa ajili ya utambulisho tayari yuko Dar na kila kitu kimemalizika kilichobaki ni wao kumta mbulisha tu,” kilisema chanzo hiko.
Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa baadhi ya wachezaji waliosajiliwa na Yanga wamehsindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu kikosini.
Atacheza kweli!
Wapo waliowahi kutua kwa matarajio makubwa lakini wakashindwa kupata dakika za kutosha kutokana na ushindani uliopo ndani ya timu hivyo mchezaji huyu kutokana na umri wake anatakiwa kuhakikisha anaonyesha kiwango cha juu uwanjani, nidhamu bora nje na ndani ya uwanja na kuyafanyia kazi maagizo ya makocha wake.
Miongoni mwao waliosajiliwa Yanga na kukosa nafasi ya kudumu kikosini ni pamoja na Shekhan Khamis, ambaye licha ya kuonekana kuwa na kipaji kikubwa, ameshindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi. Taarifa zinaeleza kuwa Yanga ipo katika hatua za mwisho za kumtoa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars, hatua itakayomsaidia kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara na kuendelea kukua.