Iran imesimamisha utekelezaji wa ahadi zake chini ya Mkataba wa Islamabad.
Akifafanua suala hilo, Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema kuwa baada ya Marekani kukiuka wajibu wake chini ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad, Tehran imesimamisha utekelezaji wa ahadi zake zote na kwamba sasa imejikita katika mipango ya kulinda nchi kwa uthabiti mkabala wa hujuma za adui.

Gharibabadi amebainisha kuwa awali Iran ilikuwa katika njia ya mazungumzo lakini Marekani ikakiuka wazi wazi ahadi zake chini ya makubaliano hayo kupitia vitendo vya uchokozi. Akijibu swali kuhusu uwezekano wa Iran kurejea kwenye meza ya mazungumzo, Gharibabadi amesema katika mazingira ya sasa, Iran inajishughulisha na mipango ya kulinda nchi dhidi ya uchokozi, na kwamba kipaumbele kikubwa kwa sasa ni kukabiliana na vitendo vya hujuma vya Marekani. Mnamo tarehe 8 Julai, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa NATO mjini Ankara Uturuki, Rais Donald Trump wa Marekani alidai kuwa kushirikiana na viongozi wa Iran ni kupoteza wakati, na akatangaza hadharani kuwa Mkataba wa Islamabad pamoja na makubaliano ya kusitisha mapigano havikuwa na maana tena.

Mkataba wa Islamabad, uliotiwa saini tarehe 18 Juni 2026 kupitia upatanishi wa Pakistan kwa lengo la kumaliza vita vya miezi kadhaa kati ya Iran na Marekani, ulikuwa na vipengele 14 na ulilenga kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya amani ya kudumu.

Kwa mtazamo wa Tehran, Marekani haijakataa tu kutekeleza masharti ya mkataba huo, bali pia imeuvunja yenyewe kwa kuanzisha tena mashambulizi ya kijeshi dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran. Uamuzi huu umefanywa ili kukabiliana na hatua za Marekani na kunufaika na haki ya kujibu uchokozi. Katika ujumbe wa hivi karibuni kuhusiana na suala hilo, Ayatullah Seyyed Mojtaba Hosseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema: “Ukiukaji wa mara kwa mara unaofanywa na ‘Shetani Mkubwa’ kuhusu makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Marais wa Iran na Marekani kwa mara nyingine tena umemthibitishia kila mtu duniani namna saini ya Rais wa Marekani isivyokuwa na thamani wala itibari yoyote, na kwamba utumiaji mabavu, ukatili na udhalilishaji wa Marekani ni miongoni mwa mambo ya yasiyotenganishika na tabia na mwenendo wa nchi hiyo.”

Ingawa Marekani ilikuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya Iran katika kipindi kilichofuatia tangazo la kusitisha mapigano, lakini kuanzia Julai 2026, ilizidisha pakubwa mashambulio hayo kwa kulenga maeneo mbalimbali katika ardhi ya Iran.

Awali, Washington ilidai kuwa ilikuwa inalenga maeneo ya kijeshi pekee, kama vile mitambo ya rada na mawasiliano, maeneo ya makombora ya ulinzi wa pwani, vifaa vya majini, na kambi za jeshi, ili kuizuia Iran kuendelea kuzuia usafiri wa meli katika Lango-Bahari la Hormuz, lakini mashambulizi ya hivi karibuni yamelenga wazi miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na madaraja, maeneo ya umma na makazi, mitambo ya maji na nishati, pamoja na miundomsingi muhimu ya pwani.

Hossein Kermanpour, Mkuu wa Kituo cha Uhusiano wa Umma na Habari katika Wizara ya Afya ya Iran, alisema Jumamosi kuwa watu 500 wamejeruhiwa na wengine 50 kuuawa shahidi katika mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani yaliyofanyika kati ya tarehe 27 Juni na 18 Julai.

Vitendo hivi vya kichokozi vinavyofanywa na Marekani ni ukiukaji wa wazi wa Ibara ya 2, Kipengee cha nne cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kanuni za msingi za mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya nchi, pamoja na marufuku dhidi ya matumizi ya vitisho na mabavu dhidi ya nchi huru. Zaidi ya hayo, mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya mali na maeneo ya raia, hasa mitandao muhimu ya usafiri na reli, ni miongoni mwa jinai za kivita.

Mbali na marufuku ya matumizi ya nguvu, namna mashambulizi hayo yanavyotekelezwa ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa za ubinadamu, ikiwa ni pamoja na Mikataba minne ya Geneva iliyopasishwa mwaka 1949.

Inaonekana kuwa lengo la Marekani la kushambulia miundombinu ya Iran ni kujaribu kubadilishana mlingano wa nguvu katika eneo hasa kuhusiana na Lango-Bahari la Hormuz, na kuilazimisha Tehran isalimu amri mbele ya matakwa ya kibabe ya Washington, hasa kuhusu suala la nyuklia la Iran. Hata hivyo, hatua madhubuti na kali za Iran dhidi ya vitendo vya uhasama vya Washington, pamoja na mashambulizi yake makali ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za Marekani katika eneo, ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa na vifo au majeraha kwa askari wa Wamarekani, bila shaka yamemthibitishia wazi Trump kuwa taifa la Iran kamwe halitapigishwa magoti na matakwa pamoja na mashinikizo ya kidhalimu ya watawala wa Marekani, si waliopita, wa sasa wala wanaokuja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *