
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei amesema kuwa Marekani imeonyesha kwa mara nyingine tena sera yake ya uharibifu baada ya kufanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya Iran.
Baqaei amesema hatua hiyo inaakisi kile alichokiita mantiki ya uharibifu inayotumiwa na Marekani katika kushughulikia masuala ya kimataifa, na akaeleza kuwa mashambulizi hayo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki ya nchi kujilinda.
Baqaei ameyasema hayo leo katika katika mkutano wake wa kawaida wa kila wiki na waandishi wa habari, alipokuwa akizungumzia vita kati ya Marekani na Iran.
Baqaei ameeleza kuwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran yamelenga maeneo ya kiraia na miundombinu isiyo ya kijeshi katika baadhi ya maeneo ya nchi hii, jambo alilosema limeonyesha tena kile alichokiita “mantiki ya uharibifu ya Marekani.”
Amesema kuwa kushambuliwa miundombinu siyo tu ni kulenga maeneo machache kwenye ramani, bali ni shambulio dhidi ya usalama wa binadamu na maisha ya watu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amezungumzia kutotimiza ahadi Marekani katika masuala ya diplomasia na mazungumzo na kubainisha kwamba, si sahihi kufikiri kwamba diplomasia inapinga ulinzi wa taifa, au kwamba ulinzi hauwezi kuendana na diplomasia.
Amesema: “Diplomasia na ulinzi ni mbawa mbili. Ikiwa moja kati ya hizo haitatimiza jukumu lake, basi jukumu la uongozi wa nchi halitatekelezwa ipasavyo.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baqaei, amesema kuwa jukumu la kuzuia kuenea vita katika eneo hilo linabebwa kikamilifu na Marekani.
Baqaei amesema kuwa Marekani inaendelea na mashambulizi yake kwa kusisitiza kutumia maeneo ya nchi za ukanda huu, jambo alilosema ni kukiuka heshima na mamlaka ya nchi hizo.
Msemaji huyo ameongeza kuwa Iran inatarajia nchi za eneo hilo kutekeleza wajibu wao na kuzuia kutumiwa ardhi yao na Marekani kwa ajili ya kufanya mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.