
Dodoma. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage ameachiwa kwa dhamana baada ya kukaa mahabusu kwa siku 14.
Kaijage alikuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, jijini Dodoma, tangu Julai 8, 2026, akituhumiwa kuhamasisha maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7, 2026.
Tangu alipokamatwa, ndugu zake pamoja na uongozi wa Umoja wa Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa) walifanya jitihada za kumwekea dhamana bila mafanikio. Hatimaye waliwasilisha maombi mahakamani, ambapo leo mahakama iliamuru apewe dhamana.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Julai 21, 2026, Mwenyekiti wa Udomasa, Dk Gerald Shija amethibitisha kuwa mwanachama wao ameruhusiwa kwa dhamana katika shauri lililokuwa mbele ya Jaji Joachim Tiganga.
“Hivi sasa tunakamilisha taratibu lakini Mheshimiwa Jaji tayari ametupa kibali cha dhamana, hivyo muda si mrefu atatoka,” amesema Dk Shija.
Katika maombi hayo, Udomasa iliwakilishwa na jopo la mawakili wakiongozwa na Wakili Prosper Malangalila, huku Kaijage akiendelea kushikiliwa mahabusu wakati shauri la dhamana likisikilizwa.
Kwa mujibu wa Dk Shija, hatua iliyopatikana ni dhamana ambayo ndiyo walikuwa wakiipigania, huku akibainisha kuwa hatua nyingine zitafuata kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amesema upelelezi kuhusu tuhuma zinazomkabili mhadhiri huyo ulikuwa unaendelea na kwamba hatua nyingine zingechukuliwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Kukamatwa na kuendelea kushikiliwa kwa Kaijage kulizua sintofahamu, huku viongozi wa Serikali na Chuo Kikuu cha Dodoma wakieleza kutokuwa na taarifa rasmi kuhusu tukio hilo na badala yake kudai walikuwa wakilipata kupitia mitandao ya kijamii.