Hai. Mlinzi wa Shule ya Msingi Mailisita, iliyopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Metivoi (25), amefariki dunia katika tukio linalodhaniwa kuwa la kujiua kwa kujinyonga.

Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni msongo wa mawazo.

Marehemu, ambaye alikuwa mkazi wa Kijiji cha Lemanyata wilayani Hai, alikutwa amening’inia kwenye dari la moja ya madarasa ya shule hiyo, akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema lilitokea Julai 20, 2026, katika moja ya madarasa ya Shule ya Msingi Mailisita.

“Tukio hili limetokea Julai 20, 2026, saa 1:00 asubuhi katika Shule ya Msingi Mailisita iliyopo Kijiji cha Maili Sita, Kata ya Mnadani, Tarafa ya Lyamungo, Wilaya ya Hai. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo kinachohisiwa kusababisha tukio hili ni msongo wa mawazo wa muda mrefu,” amesema Kamanda Maigwa.

Aidha,  Kamanda Maigwa amesema uchunguzi zaidi wa tukio hilo  unaendelea ili  kubaini mazingira yote ya tukio hilo.

Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai ukisubiri uchunguzi wa kitaalamu na taratibu nyingine.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Shiri Njoro,  Alfonsina Otari amesema wananchi wamepatwa na mshangao kwani miezi mitatu iliyopita mlinzi mwingine wa  shule hiyo alikutwa amefia  ndani ya kihenge cha kuhifadhi mahindi.

“Kinachotushangaza zaidi miezi mitatu iliyopita kuna  mlinzi mwingine wa shule hii alikutwa  amefariki ndani ya kihenge cha mahindi, tumebaki na mshangao maana hatujakaa muda mrefu mlinzi mwingine kafariki kwa  kujinyonga, sijui ni kitu gani kimetokea kwenye hii shule,” amesema Otari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *