
Dar es Salaam. Wahitimu wa vyuo vikuu katika fani ya ualimu watalazimika kufanya mafunzo ya kazi yanayolenga kujenga uzoefu wa kitaaluma (internship) kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuhitimu, kabla ya kupatiwa leseni ya kufundisha.
Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Lyabwene Mtahabwa, amethibitisha kuwapo kwa utaratibu huo, akisema ni sehemu ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ulioboreshwa nchini.
Katika kufuatilia utekelezaji wa mfumo huo, leo Jumanne, Julai 21, 2026, Mwananchi imezungumza na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa, ambaye amesema utaratibu huo hautafuta mafunzo ya ufundishaji kwa vitendo yanayofanywa na wanafunzi wakiwa vyuoni.
Amesema wanafunzi wataendelea kufanya mafunzo ya ufundishaji kwa vitendo shuleni chini ya usimamizi wa wakufunzi wa vyuo na walimu wa shule, huku wakiendelea na masomo yao katika mihula husika.
“Utaratibu ni kwamba watakuwa wanakwenda kujifunza kufundisha kwa vitendo wakisimamiwa na walimu wa chuo pamoja na walimu waliopo shuleni, huku wakiendelea na masomo yao katika muhula, kama ambavyo wanafunzi wa udaktari hufanya clinical rotation (mzunguko wa mafunzo ya kliniki),” amesema Profesa Kihampa.
Amesema baada ya kuhitimu masomo yao, wahitimu hao watafanya mafunzo ya kazi kwa mwaka mmoja kabla ya kupatiwa leseni ya kufundisha.
“Baada ya kumaliza masomo watafanya internship ya mwaka mmoja, ndipo wapatiwe leseni,” amesema Profesa Kihampa.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Goodluck Francis, akizungumza na Mwananchi amesema utaratibu huo tayari umeelezwa kwa wanafunzi, lakini utaanza kutumika kwa waliojiunga mwaka wa kwanza.
“Sisi wa mwaka wa tatu tumeambiwa hautatuhusu. Utaratibu wa kwenda kujifunza kwa mwaka mmoja utaanza kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Hii ni fursa nzuri kwa wanafunzi kupata uzoefu wa muda mrefu wa kazi na kujifunza hali halisi ya mazingira ya kufundishia,” amesema.
Malipo ya walimu wanaofanya mafunzo
Akizungumzia malipo ya wahitimu watakaokuwa kwenye mafunzo hayo ya mwaka mmoja, Profesa Kihampa amesema suala hilo haliko chini ya mamlaka ya TCU.
Hata hivyo, Mwongozo wa Walimu wa Kujitolea katika Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania Bara wa Juni 2023, unaeleza kuwa rasilimali za utekelezaji wa programu hiyo zitatokana na ushirikiano wa Serikali, wazazi na wadau wa maendeleo.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, halmashauri zitatumia mapato yake ya ndani kulipa posho kwa walimu wanaofanya mafunzo hayo kulingana na uwezo wa kifedha na mahitaji yaliyopo.
Mwongozo huo pia unaeleza kuwa fedha za kugharamia programu zinaweza kupatikana kupitia shughuli za elimu ya kujitegemea zinazofanyika shuleni au katika vyuo vya maendeleo ya wananchi, pamoja na michango ya wadau wa maendeleo na watu binafsi.
Kauli za wanafunzi na wakufunzi
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), aliyeomba kutotajwa jina lake, amesema tayari wamejulishwa kuhusu utaratibu huo mpya.
“Tumeambiwa huu ni mfumo mpya. Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja tutakuwa tunapata malipo kidogo huku tukiendelea kujifunza. Bila kufanya mafunzo hayo huwezi kukamilisha utaratibu, hutakuwa na sifa zinazohitajika,” amesema.
Mkufunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), ambaye pia hakutaka kutajwa jina lake, amesema maandalizi ya utekelezaji wa mfumo huo yanaendelea.
“Bado haujaanza kutekelezwa, lakini tayari tumepewa taarifa tujiandae. Pia tumeelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatarajiwa kuanza utekelezaji wake mwaka ujao,” amesema.
Kwa upande wake, mwanafunzi mwingine wa UDSM amesema amekuwa akisikia taarifa kuhusu utaratibu huo kutoka kwa wanafunzi wenzake, ingawa bado hajapata taarifa rasmi kutoka chuoni.
Wataalamu waeleza manufaa
Mtafiti wa elimu, Dk Muhanyi Nkoronko, amesema mfumo huo unaweza kuongeza ubora wa walimu wanaohitimu kwa kuwapa muda wa kutosha wa kujifunza mazingira halisi ya kazi kabla ya kuanza kufundisha rasmi.
Amesema tofauti na mfumo wa sasa unaowapa wanafunzi muda mfupi wa mafunzo ya ufundishaji kwa vitendo, mafunzo ya mwaka mzima yatawawezesha kukabiliana na changamoto za kazi na kujifunza mbinu bora kutoka kwa walimu wenye uzoefu.
“Kwa kukaa shuleni kwa mwaka mzima, mwalimu mtarajiwa atapata nafasi ya kujifunza kwa kina zaidi. Atakutana na changamoto halisi za darasani, atajifunza namna ya kuzitatua na kupata maarifa ya kutosha kutoka kwa walimu waliobobea. Hii itaimarisha uwezo wake wa kufundisha na hatimaye kuongeza ubora wa elimu,” amesema.
Kwa upande wake, mhitimu wa ualimu wa mwaka 2020, Emmanuel Kamenge, amesema mfumo huo unaweza kusaidia kupunguza uhaba wa walimu kwa kuongeza idadi ya walimu watakaokuwa shuleni kupitia mafunzo ya kazi.
Hata hivyo, amesema baadhi ya wahitimu wa miaka iliyopita wana hofu kuwa utaratibu huo unaweza kuongeza ushindani katika ajira.
“Mfumo huu una faida, lakini kwa sisi tuliomaliza miaka ya nyuma unaweza kufanya upatikanaji wa ajira kuwa mgumu zaidi, kwa sababu wahitimu wapya watakuwa tayari wako shuleni wakifanya mafunzo ya mwaka mmoja kabla ya kukamilisha taratibu zote za taaluma,” amesema.