Morogoro. Mtu mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya lori lililobeba kemikali aina ya salfa kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba mchanga, kisha lori hilo la mchanga kushika moto na kuteketea katika ajali iliyotokea alfajiri ya leo, Julai 24, 2026, mkoani Morogoro.

Ajali hiyo imetokea eneo la Mafiga kwenye Barabara Kuu ya Morogoro–Iringa, ikiwa ni takribani miezi miwili tangu kutokee ajali nyingine iliyohusisha lori lililobeba kemikali katika eneo la Mindu kwenye barabara hiyo, hali inayoibua wasiwasi kuhusu usalama wa magari makubwa yanayotumia njia hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo amesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:00 alfajiri ikihusisha lori aina ya Scania, lililokuwa likisafirisha kemikali aina ya salfa kutoka Dar es Salaam kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na lori jingine lililokuwa limebeba mchanga kutoka Lugono kuelekea Chalinze.

Kemikali aina ya salfa ikiwa imemwagika barabarani baada ya lori lililokuwa limebeba kemikali hiyo kugongana na lori la mchanga na kisha kuwaka moto eneo la Mafiga, barabara ya Morogoro–Iringa, alfajiri ya Julai 24, 2026. Picha na Hamida Shariff.

Amesema baada ya magari hayo kugongana, lori la mchanga lilishika moto na kusababisha mmoja wa waliokuwemo ndani yake, mwanaume mtu mzima ambaye bado hajatambulika, kufariki dunia kwa kuungua.

“Kutokana na mgongano huo, lori la mchanga lilishika moto. Mmoja wa waliokuwemo kwenye lori hilo amefariki dunia na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro,” amesema Kamanda Kantimbo.

Amesema watu wengine wawili, Wilson Samson na utingo wake, Meshack Mushi, walijeruhiwa katika ajali hiyo na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro wakimalizia zoezi la kuzima moto ulioteketeza lori la mchanga lililopata ajali baada ya kugongana na lori lililobeba kemikali eneo la Mafiga, barabara ya Morogoro–Iringa, alfajiri ya Julai 24, 2026. Picha na Hamida Shariff.

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa ajali hiyo ilitokana na lori la mchanga kujaribu kulipita gari jingine bila kuchukua tahadhari, kabla ya kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa likitokea upande wa pili.

Hamis Digilo, mmoja wa mashuhuda, amesema dereva wa lori la mchanga alionekana kuanza kulipita gari dogo, lakini hakufanikiwa kurejea kwenye njia yake kwa wakati.

“Alikuwa analipita gari dogo, lakini hakupata nafasi ya kurudi kwenye njia yake ndipo akagongana na lori lililobeba salfa. Baada ya hapo lori la mchanga likaanza kuwaka moto,” amesema.

Amesema askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto walifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kuuzima moto pamoja na kurejesha hali ya usalama barabarani.

Shuhuda mwingine, Juma Msangi amesema kishindo cha ajali hiyo kiliwashtua wakazi wa eneo hilo waliokimbilia eneo la tukio, lakini moto mkubwa uliokuwa ukiwaka ulifanya juhudi za uokoaji kuwa ngumu.

“Hali ilikuwa ya kutisha. Tulifika tukakuta lori moja tayari linawaka moto na wananchi walikuwa wanajaribu kusaidia, lakini moto ulikuwa mkubwa sana,” amesema.

Kwa upande wake, mkazi wa Mafiga, Abdul Kamga amesema ajali hiyo inapaswa kuwa fundisho kwa madereva wa magari ya masafa marefu, akiwataka kutolazimisha kuendelea na safari wanapohisi uchovu au usingizi.

“Madereva wanapohisi wamechoka wasiendelee na safari kwa lazima. Wapumzike kwanza kwa sababu uchovu unaweza kusababisha maamuzi mabaya yanayogharimu maisha,” amesema.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, huku likiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan wakati wa kulipita gari lingine kwenye barabara kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *