
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, watu wa Iran wamesimama imara mitaani hadi ushindi wa mwisho.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo katika hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa katika Musalla wa Imam Khomeini na kuwahutubu wananchi wa Iran akisema: “Enyi wananchi wavumilivu wa Iran, kwa muda wa siku 145 (karibu miezi mitano) hamjaondoka mitaani, na bado mnaendelea kusimama humo kwa uthabiti, bila kuchoka, hadi ushindi wa Uislamu.”
Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, mikusanyiko ya wananchi mitaani ni miongoni mwa ibada za wazi za watu wa Iran, akisema:”Kwa hakika ninyi wananchi wenye uvumilivu wa Iran mtashinda, na maadui watashindwa.”
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran akieleza kwamba ndani ya Qur’ani Tukufu yametajwa majina 70 ya Siku ya Kiyama, amesema kuwa miongoni mwa majina hayo ni “Yawmul-Hisab” (Siku ya Hisabu), yenye maana kwamba kila jambo ambalo wanadamu tunalifanya duniani, tutalazimika kutoa hesabu yake huko Akhera.
Akisisitiza kwamba katika mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w) suala la muuqawama kusimama imara lilikuwa jambo lililopewa umuhimu mkubwa, amesema: “Kusimama katika njia ya haki na kutorudi nyuma kutoka kwenye njia hiyo kunahusishwa na maneno matatu ya Qur’ani Tukufu: subira, uthabiti na kusimama imara.”
Ayatullah Khatami amesema, Mtume (SAW) pamoja na Maswahaba zake walisimama kidete kwa miaka 23 na hawakuacha hata kidogo njia ya haki.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo Tehran amesema, vijana wanapaswa kuzingatia kwamba kulikuwa na kundi fulani katika mwanzo wa historia ya Uislamu lililojulikana kama “Mu’adhabina Fillah”, yaani watu walioteswa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ambao walivumilia mateso hayo na kubaki imara.
Ameeleza kuwa miongoni mwao walikuwa watu saba wanaume na sita wanawake. Ameongeza kuwa wanawake wa leo wanapaswa kufahamu kwamba wanawake katika zama za mwanzo za Uislamu walisimama pamoja na wanaume katika kupambana na dhuluma; walitoa maisha yao lakini hawakuacha misingi ya imani na malengo yao. Walivumilia na kusimama imara hadi tone la mwisho la damu kwa ajili ya itikadi zao.