Dar es Salaam. Moja ya kauli zinazosikika mara kwa mara katika jamii ni kwamba mtu mwenye kisukari haruhusiwi kula sukari kabisa.

Wapo wanaoamini hata tunda lenye utamu, kipande cha keki au kijiko cha sukari kwenye chai kinaweza kuwa “sumu” kwa mgonjwa wa kisukari.

Imani hii imekuwepo kwa miaka mingi, lakini ukweli ni tofauti kidogo na jinsi watu wengi wanavyofikiri.

Ni muhimu kuelewa ni kisukari si ugonjwa unaotokana na kula sukari pekee. Kisukari ni hali inayohusisha mwili kushindwa kuzalisha insulini ya kutosha au kushindwa kuitumia vizuri.

Hivyo, matibabu na lishe ya mtu mwenye kisukari hulenga kudhibiti kiwango cha sukari si kuharamisha chakula fulani moja kwa moja.

Mtu mwenye kisukari anaweza kula vyakula vyenye sukari au mafuta kwa kiasi kinachofaa na kwa kuzingatia mpango wa lishe aliopangiwa.

Hakuna sheria inayosema kuwa kipande kidogo cha keki kwenye sherehe au kijiko cha sukari kwenye chai ni marufuku kwa kila mtu mwenye kisukari. Muhimu ni kujua kiasi unachokula na kiwango cha sukari yako muda huo.

Kwa mfano, mtu mwenye kisukari aina ya kwanza anayetumia insulini anaweza kula vyakula vyenye wanga au sukari kwa kupanga dozi ya insulini kulingana na ushauri wa mtaalamu wa afya.

Vivyo hivyo, mtu mwenye kisukari aina ya pili anaweza kufurahia baadhi ya vyakula hivi kwa kiasi, huku akizingatia ulaji wa mboga, protini, nafaka zisizokobolewa na kufanya mazoezi.

Vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta mengi na kalori nyingi vikiliwa mara kwa mara na kwa kiasi kikubwa, vinaweza kufanya udhibiti wa sukari kuwa mgumu, kuongeza uzito na kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo. Hivyo, suala si kukataza kabisa, bali ni kula kwa kiasi na kwa busara.

Tatizo lingine linalotokana na imani hii potofu ni kwamba baadhi ya watu hujikuta wakiepuka sukari kabisa hata pale sukari inaposhuka sana na ni hatari, hasa kwa watu wanaotumia insulini au baadhi ya dawa za kisukari.

Wakari sukari imeshuka sana mwili huhitaji sukari ya haraka ili kurejesha kiwango cha kawaida cha sukari kwenye damu.

Udhibiti wa kuishi na kisukari hautokani na kuogopa kula sukari pekee bali unategemea lishe yenye uwiano, kufanya mazoezi, kutumia dawa, insulini kama ulivyoelekezwa, kufuatilia kiwango cha sukari kwenye damu na kuhudhuria kliniki mara kwa mara.

Elimu sahihi ndiyo njia bora ya kuvunja imani potofu. Badala ya kuwaambia watu wenye kisukari kwamba “msile sukari kabisa”, ni bora kuwafundisha namna ya kula kwa kiasi, kupanga milo yao na kufanya uamuzi sahihi kila siku.

Hiyo ndiyo njia inayowawezesha kuishi maisha yenye afya bila hofu wala vikwazo visivyo na msingi wa kisayansi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *