Wakati juhudi za kimataifa na kitaifa za kudhibiti ugonjwa wa kichocho zikijikita zaidi kwa wanafunzi wa shule za msingi na watu wazima, Tanzania sasa inapiga hatua kubwa kuelekea kuwajumuisha watoto walio chini ya umri wa kwenda shule katika mfumo wa matibabu na kinga.

Hali hiyo inakuja kufuatia kukamilika kwa utafiti uitwao: National Consensus on Introducing and Delivery of Paediatric Praziquantel for Curative and Preventive Treatment of Schistosomiasis Among Pre-school Children in Tanzania.

Utafiti huo umelenga kuandaa mfumo wa afya nchini kwa ajili ya mapokezi na usambazaji wa dawa mpya ya kichocho (arPZQ) iliyotengenezwa maalum kwa ajili ya watoto wadogo, ambayo ilitarajiwa kuanza kupatikana sokoni tangu mwaka 2025.

Kwa muda mrefu, watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wamekuwa wakisahaulika katika kampeni za kutoa dawa za kinga, jambo lililosababisha mahitaji makubwa ya mfumo maalum wa kuwafikia watoto hao.

Utafiti huu wa kimkakati ulihusisha mikutano ya mashauriano, majadiliano ya vikundi, na ushirikishwaji wa wadau kuanzia ngazi ya taifa hadi jamii.

 Kupitia mchakato huo, wadau waliibua changamoto na mapengo yanayoweza kukwamisha uanzishwaji wa dawa hiyo na kutafuta suluhu mapema.

Mifumo ya usambazaji Iliyopendekezwa

Ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma, mwafaka wa kitaifa uliofikiwa unapendekeza njia kuu tatu za kuwafikishia watoto dawa hizo.

Mosi, katika jamii: Kuwafikia watoto majumbani na katika maeneo yao.

Pili, vituo vya afya: Kuwapatia dawa watoto wanaofika kliniki kwa ajili ya huduma za kawaida za afya au ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto.

Tatu, kampeni maalum: Kutumia kampeni zilizopo, kama zile za kutoa matone ya Vitamin A, kama fursa ya kutoa dawa hizo za kichocho.

Pamoja na mwafaka huo, utafiti unasisitiza kuwa kabla ya kuanza rasmi usambazaji wa dawa hiyo ya Paediatric Praziquantel, ni lazima kuimarisha uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya.

“Kabla ya kuanza kutoa dawa hii, uwezo wa vituo unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha wahudumu wa afya wanakuwa na ujuzi sahihi na wanafanya kile kinachostahili wakati wa utoaji wa dawa,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hatua hii ya Tanzania inaelezwa kuwa itakuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikilenga kutokomeza kabisa kichocho, ambacho kimekuwa kikiathiri ukuaji na afya ya watoto wengi katika maeneo yenye vyanzo vya maji.

Kijue kichocho

Ugonjwa wa kichocho ni mojawapo ya magonjwa yanayoshambulia watu wengi hasa katika maeneo ya vijijini na miji inayotumia maji machafu.

Ugonjwa huu ni hatari kwa afya ya binadamu, kwani unashambulia mwili hasa mfumo wa mkojo na mifupa, na unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa hautatibiwa mapema.

Kichocho husababishwa na minyoo ya aina ya Schistosoma, ambayo hutegemea mwili wa binadamu na mazingira ya maji kwa mzunguko wake wa maisha. Minyoo hii hupatikana katika maji ya asili kama mabwawa, maziwa, mito na maeneo ya maji yanayotumika na binadamu kwa shughuli kama kuogelea, kupiga mbizi au kunywa maji. Wakati binadamu anapogusa au kuingia kwenye maji yenye minyoo ya Schistosoma, vimelea hivyo huingia mwilini kupitia ngozi na kuhamia kwenye mzunguko wa damu. Minyoo hukua na kuzaa kisha hujielekeza katika viungo mbalimbali kama figo, kibofu cha mkojo, na ini, na hapa ndipo dalili za ugonjwa huu huonekana.

Dalili za kichocho hutofautiana kulingana na aina ya bakteria  wanaosababisha maambukizi. Hata hivyo, baadhi ya dalili kuu ni pamoja na maumivu ya tumbo, uchovu, homa, mkojo wenye damu, magonjwa ya ini na mifupa.

Wakati mwingine, dalili za kichocho zinaweza kutokea miezi au hata miaka baada ya kuambukizwa, jambo linalofanya ugonjwa huu kuwa ngumu kugundulika mapema. Ikiwa hautatibiwa mapema, kichocho kinaweza kusababisha madhara makubwa kama uharibifu wa figo, ini, na matatizo ya uzazi hasa kwa wanawake.

Kichocho hutokana na mawasiliano ya moja kwa moja na maji yenye minyoo ya Schistosoma. Maambukizi hutokea wakati binadamu anapogusa maji yenye minyoo au anaposhiriki shughuli kama kuogelea, kupiga mbizi, au kunywa maji yaliyotumika na wanyama au watu wa maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huu. Maji machafu ni chanzo kikuu cha maambukizi, na matumizi ya maji kwa shughuli za kilimo au shambani pia ni hatari kwani yanaweza kueneza vimelea vya minyoo hii.

Matibabu na kinga

Kichocho ni ugonjwa unaoweza kutibiwa kwa urahisi endapo utagundulika mapema. Dawa maarufu inayotumika kutibu kichocho ni Praziquantel, inayosaidia kuua minyoo ya bakteria na kupunguza madhara yanayoweza kutokea kwa mtu aliyeambukizwa.

Dawa hii hutolewa na vituo vya afya na hospitali, na inapatikana bure kwa watu walioathirika katika maeneo ya hatari.

Kwa upande wa kinga, njia bora ni kuepuka kuingia kwenye maji machafu na kutumia maji safi na salama kwa shughuli za kila siku.

Kinga nyingine ni pamoja na kutibu maji yanayotumika kwa kilimo au shambani, kuboresha huduma za maji safi, na kuwafundisha wananchi kuhusu hatari za kichocho na njia za kujikinga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *