
Dar es Salaam. Simba imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao ambapo leo Ijumaa, Julai 24, 2026 imetangaza kumnasa mshambuliaji raia wa Mali, Ibrahim Doumbia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, amejiunga na Simba akitokea AS Korofina inayoshiriki Ligi Kuu ya Mali.
Uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho unaonekana kuchangia kuishawishi Simba iingie sokoni na kumsajili mshambuliaji huyo.
Msimu uliopita, Doumbia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Mali ambapo alifunga mabao 17 na kupiga pasi tano za usaidizi wa mabao.
Mchezaji huyo pia amecheza idadi ya mechi 26 za timu ya taifa ya vijana ya Mali chini ya umri wa miaka 20 na kupachika mabao 22.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na usajili tunaofanya umezingatia matakwa hayo,” imesema taarifa ya Simba.
Doumbia anakuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kutambulishwa na Simba katika dirisha hili kubwa la usajili wa wachezaji linaloendelea nchini.
Timu hiyo hadi sasa imeshatambulisha wachezaji watatu wazawa ambao imewasajili hivyo kiujumla, Doumbia anakuwa mchezaji wa nne kutambulishwa.
Kabla ya Doumbia, wachezaji wengine ambao Simba imeshawatambulisha ni Nathanaiel Chilambo, Bakari Msimu na Kelvin Nashoni.