Mwanza. Taharuki imetokea leo Ijumaa Julai 24, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, baada ya ndugu wa marehemu Wambura Mumbiya (54) kugombea mwili, kila upande ukitaka kumzika.

Tukio hilo limetokea baada ya mke mkubwa wa marehemu, Elizabeth Nyakao kupata taarifa kuwa ndugu wa mume wake wamepanga kumzika kwa mke mdogo.

Akizungumza nje ya hospitali hiyo, Elizabeth amesema ameishi na mume wake kwa miaka 32, lakini baadaye akabadilika na kuitenga familia hiyo kwa miaka 5.

Amesema ndugu wa mume wake wanang’ang’ania mume wake akazikwe kwa mke mdogo ambaye anasema hajawahi kumjua.

“Kinachoniumiza mume wangu nataka niende nikamzike shemeji yangu ananikatalia…anataka mwili ukazikwe kwa bibi mdogo na mimi sitaki,” amesema.

Gladson Mambiya, kaka wa marehemu akizungumzia mgogoro wa kugombea mwili wa marehemu. Picha na Saada Amir

Binti mkubwa wa marehemu, Happiness Wambura amesema walishtushwa na taarifa za siri za kuuchukua mwili wa baba yao bila kuwahusisha na kuamua kufika hospitalini hapo kuzuia.

“Tulipata taarifa kuwa kuna mpango wa kuuchukua mwili wa baba yetu bila sisi kujua. Hilo lilitushtua sana, ndiyo maana tukaja hapa haraka kuzuia jambo hilo,” amesema.

Nakuongeza, “Tunachotaka ni tukabidhiwe baba yetu tukamzike kwa heshima…hatuwezi kukubali azikwe nje ya familia yake.”

Ameongeza kuwa baba yao alikuwa akiugua kwa miezi sita kabla ya kufariki dunia, na mara nyingi alikuwa akiishi visiwani kutokana na kazi yake ya uvuvi.

“Baba alikuwa mvuvi, muda mwingi alikuwa visiwani. Ameacha watoto saba na wajukuu sita…tunahitaji kuona anaondoka kwa heshima anayostahili,” ameeleza.

Kaka wa marehemu na msemaji wa familia, Gradson Mambiya amesema chanzo kikuu cha mgogoro huo ni ukweli kwamba marehemu alikuwa na wake wawili, wote wakiwa na watoto naye.

“Uhalisia ni kwamba mdogo wangu alikuwa na wanawake wawili na wote ni wake zake halali kwa namna yao…Tatizo lililopo sasa ni nani atazika, na hapa ndipo mgogoro ulipoanzia,” amesema.

Ameeleza kuwa kabla ya kifo chake, marehemu aliwahi kutoa maelekezo kuhusu mahali alipotaka kuzikwa kuwa azikwe kwa bibi mdogo.

“Marehemu alituambia wazi kabisa kuwa akifa hataki kuzikwa kwa mke mkubwa, alitaka azikwe kwa mke mdogo. Mimi binafsi aliniambia, na ndugu wengine pia wanajua hilo,” amesema.

Elizabeth Nyakao, mke mkubwa wa marehemu akizungumza nje ya Hospitali ya Sekou Toure. Picha na Saada Amir

Hata hivyo, amesema mke mkubwa hakukubaliana na kauli hiyo na alisisitiza kuwa ana haki ya kushiriki kikamilifu katika mazishi ya mume wake.

“Baada ya kifo, tulimweleza mke mkubwa kuhusu kauli ya marehemu, lakini amekataa…sasa kwa sababu wote ni wake zake, sisi kama familia tumeona bora mwili uzikwe nyumbani Musoma ili kuepusha mgogoro,” ameeleza.

Amesema uamuzi huo unalenga kuhakikisha hakuna upande unaojihisi kutengwa au kunyimwa haki.

“Tunataka kila mtu aridhike. Huyu alikuwa ndugu yetu, hatutaki azikwe kwa vurugu. Tunataka aondoke kwa amani, na wale waliobaki watamaliza tofauti zao baadaye,” amesema.

Akizungumza eneo la tukio, Dativa Witlaus kutoka kitengo cha utafiti cha Shirika la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza (Sinaujata), amesema walifika hospitalini hapo baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa mgogoro huo.

Amesema, “Tulipofika tulikuta tayari kuna malumbano makali kati ya Bi. Mkubwa na Bi. Mdogo, kila mmoja akitaka kupewa mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi…hali ilikuwa tete na tulilazimika kuitisha kikao cha dharura ili kujaribu kuwapatanisha.”

Amesema katika kikao hicho, pande zote zilionyesha msimamo mkali huku kila upande ukisisitiza haki yake, jambo lililofanya iwe vigumu kufikia muafaka wa haraka.

“Kwa pamoja tulikubaliana kuwa sisi kama ustawi wa jamii hatuwezi kuamua nani achukue mwili, bali tulishauri kuwepo kwa maridhiano. Tulitaka wao wenyewe wakubaliane na kutuletea majibu,” amesema.

Hata hivyo, jitihada hizo hazikuzaa matunda mara moja, kwani baada ya kutoka nje kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo, hali ilizidi kuwa mbaya.

“Tulipotoka nje, watu walikusanyika wengi, takribani 40 au zaidi. Badala ya mazungumzo, kelele zilianza, watu wakaanza kugombana, wengine wakapigana ngumi. Ilikuwa ni hali ya hatari, vumbi lilitanda na hata magari yaliyokuwa yanapita yalikuwa hatarini kugonga watu,” ameeleza.

Kwa mujibu wa Witlaus, askari waliokuwa eneo hilo walijaribu kuingilia kati lakini walikumbana na upinzani kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa na hasira.

“Askari walijitahidi lakini hali ilikuwa imechafuka sana. Ilibidi viongozi wa hospitali na watu wengine waingilie kati kuwatuliza,”amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema waliamua kuchukua hatua zaidi kwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi (Central) ili kupata msaada wa mamlaka za juu.

Naye mkazi wa jijini Mwanza, Mariam Ezekiel, amesema tukio hilo ni la kusikitisha na linapaswa kuwa funzo kwa jamii.

“Hili tukio halifurahishi kabisa. Kwa mila nyingi za Kiafrika, mwanaume anapofariki anarudishwa kwenye familia yake ya kwanza hasa kwa mke mkubwa…hata kama alikuwa na wake wengine, mazishi hufanyika hapo,” amesema.

Amesema migogoro ya aina hiyo inaweza kuepukika kama kutakuwa na utaratibu mzuri wa kisheria kwa ndoa za wake wengi ikiwemo wanaume kuandika wosia.

“Serikali inapaswa kuweka utaratibu rasmi ambapo wanaume wenye wake wengi wanaweka maandishi mapema kuhusu masuala kama haya. Itasaidia kuepusha migogoro kama hii,” ameeleza.

Hadi kufikia saa 10 jioni, juhudi za kuwapatanisha pande hizo zilikuwa bado zinaendelea huku mamlaka zikisisitiza umuhimu wa maelewano ili kuhakikisha mwili wa marehemu unazikwa kwa amani na heshima, bila kuendelea kwa vurugu zilizoshuhudiwa mapema katika hospitali hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *