Dar es Salaam. Hii ni maajabu! Bado tupo mwezi Januari? Mwezi una miezi mitatu ndani yake, kwa hiyo sasa hivi ni mwezi wa tatu ndani ya mwezi wa kwanza? Tunataka kuishi ‘kituristi gademiti’. 

Xmass imetupukutisha. Mwaka mpya umetupukutisha. Kuna ada na kodi zimetupukutisha. Tupo hoi kinoma, tumekata ringi kama ‘sista duu’ katika wodi ya wazazi, tumetepeta kama tambi.

Madeni kila kona kama serikali ya Sudan Kusini. Tumechakaa kama serikali ya Somalia. Tumefubaa kama utawala wa Libya baada ya kifo cha Gaddaf. Kimsingi mbili wala tatu hazisomi. Salaaale!

Ndani ya mwezi mmoja tumekula bata la mwaka mpya. Makonda kapewa uwaziri kamili, Kajala na Konde wamerudiana. Taifa Stars ilivuka 16 bora AFCON, Morocco wakatudhulumu penalti kenge wa bluu wale.

Ndani ya mwezi huu Gamond kapewa timu ya taifa na Chama karudi Simba. Yote haya ni ndani mwezi mmoja, achana na mambo ya sirini. Kama ‘kuchiti’ kimapenzi, kutoa mimba na kutafuna wake za watu.

Huu ndo mwezi ambao wanaume hupendwa na ‘singo maza’ kuliko mabishoo. Usawa huu ‘blazameni’ gani wa kulipa kodi ya nyumba na ada ya mtoto? Januari ni mwezi dume kwa wanaume pekee siyo wavulana.

Kuna dingi mwezi huu limelipa ada za watoto wake kadhaa. Na ada za watoto wa dada zake au nduguze tu. Ada za watoto wa michepuko ama nyumba ndogo, na kodi ya videmu kama vitatu vya Sinza na Tabata.

Halafu muda huu linakifukuzia kidem flan kipya cha Kinondoni. Au kuwadi flani limempelekea videmu kama vitatu mfululizo. Linamlipa kuwadi na linavilipa videmu vyote na bado uchumi wake uko sawa.

Das’lam mjini unatakiwa kusema sina pesa, usiseme hatuna pesa. Ni wewe peke yako na njaa njaa zako usituunganishe watu wote. Lakini uchache wa wenye ukwasi hautuzuii kusema Janauri hii ni ngumu. Ni msala huu mwezi.

Utakuta dingi linaongea kivyake ‘rodini’. Usishangae wengi wao wamepigika na ‘laifu’ ngumu ya Januari. Majukumu mengi kuliko idadi ya nywele na ndevu zake za maeneo ya wazi na yale ya sirini.

Mtu kachachuka kama mbege ya Xmass, anadaiwa ada, anadaiwa kodi. Anatakiwa kulipia sare za watoto kwa fundi Kinyanduka. Na wakati huohuo aliacha bili kibao kaunta kwenye bar ya jirani. Aisee ni kwere.

Ukimuona njiani kama binadamu kamili. Kumbe ni boksi tupu hapo akili ziko nje ya bichwa lake. Ndo maana washua ‘wanaresti ini pisi’ mapema, utadhani wanatangulia kwa ‘Saa Godi’ kuandaa nyumba ya familia yake. 

Wengi tunafanya kazi katika ofisi, idara, taasisi, kampuni, mashirika na ‘enjiyozi’ zenye uchumi tenge. Yaani bosi anatamani uache kazi, na mhasibu anatamani usahau salare yako. Mmiliki anatamani kuhama nchi. 

Unalipwa tofauti na matumizi yako. Chini ya laki tano ndo salare yako, upo Sinza, deile unalewa. Una dem wawili watatu, unatoaga ‘kipu chenji’ kwa ‘mabaamedi’, na unarudi ‘homu’ na bajaji au boda deile. 

Na asubuhi unapiga supu kibabe sana. Unashushia na biere mbili tatu kabla ya kuanza mishe zako. Na ukikikuta kijamaa flan kinalia na serekale unakichana, kwamba kifanye kazi kiache kulialia. Aisee sisi ni wa ajabu.

Kuna masela wanalipwa elfu 80 na wadosi. Mitaa ya Kariakoo au Kisutu kama siyo Mnazi Mmoja na Posta. Anaishi Kimara, Mbezi ama Kibamba ndani ndani. Deile anapanda mwendokasi kwenda jobu na anarudi kalewa.

Na kabla ya kufika kituo cha basi anatumia boda au bajaji kwenda na kurudi. Kajenga vyumba viwili mita mia nne kutoka ‘rodini’, ana mke na watoto wawili au watatu. Hakosi kazini kila siku na husikii akilalamikia mshahara mdogo. Gademiti. 

Hii nchi imejaa wezi, wazazi wezi, viongozi wezi, wafanyakazi wezi, viongozi wa kiroho wezi, malaya wezi, madereva wezi, polisi wezi na wezi ni wezi zaidi. Hakunaga mwenye nafuu hata wake zetu ni wezi.

Mwezi huu wa Januari kuna dada kalipiwa pango la nyumba na kina baba watatu hadi wanne. Na kuna dada kalipiwa ada ya watoto na wanaume wawili au watano. Na wote hawajuani kama ‘wanashea’ penzi moja. Maajabu!

Ni kama mhudumu wa bar hivi. Anahudumia meza tatu na zote kaacha bia nusu nusu, na meza zote kaahidi kuondoka na mtu. Na wote anawaibia kwa kubana chenji au kuwazidishia bili. Akili kumkichwa. 

Sina ‘memori’ nzuri kama hii ni makala ya ngapi kwa mwezi huu mmoja. Ni kama makala nane na zaidi ndani ya mwezi na hauishi niokote. Deile vizinga kwa masela hadi wananileta zogo kama vile mimi magumashi hivi.

Siyo kesi, twendeni tukalewe tu. Hii ni Jumamosi ya mwisho kwa mwezi huu wa kipimbi. Hatuna sababu ya kuacha kusherehekea kuumaliza mwezi uliojaa shida kuliko raha. Nyambafu Januari na usirudi tena, acha tuishi kituristi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *