Dar es Salaam. Tunaweza kusema siri ya mafanikio ya Darassa kimuziki imefichwa katika uwezo wake wa kuchagua wasanii wa kushirikiana naye, kitu ambacho kimemfanya kuwa rapa wa kisasa na tishio katika tasnia.

Darassa, mwanzilishi wa Classic Music Group (CMG), kwa sasa anasifika na wengi kwa namna alivyofanikiwa kubadili mtindo wa muziki wake na kuja kivingine kwa lengo la kulishika zaidi soko la muziki.  

Rapa huyu alitoka rasmi kimuziki kupitia wimbo wake, Sikati Tamaa (2012) akimshirikisha Ben Pol, kolabo iliyotayarishwa na Bob Manecky katika studio za AM Records.

Baada ya hapo, mfululizo wa nyimbo kali ndio uliochukua nafasi tena kwa miaka mingi hadi alipokuja kutoa albamu yake ya kwanza, Slave Becomes a King (2020), kisha ya pili, Take Away The Pain (2025).

Na kwa sasa Darassa ndiye rapa namba moja Bongo katika majukwaa (digital streaming) yote ya kusikiliza muziki mtandaoni ikiwemo YouTube Music, Spotify, Boomplay, Apple Music n.k.

Mathalani kwa mwaka 2024, Darassa ndiye alikuwa rapa aliyefanya vizuri zaidi YouTube ambapo kazi zake (video na audio) zilitazamwa zaidi ya mara milioni 29 ndani ya kipindi cha miezi 12.

Waliomfutia ni Billnass aliyetazamwa mara milioni 16.7, kisha Nay wa Mitego 10.6, Kontawa 8.9, Professor Jay 8.2, AY 7.7, Roma 6.5, G Nako 6, Young Killer 4.6 na Stamina 3.6.

Hata hivyo, mabadiliko na mafanikio hayo ya Darassa yanatokana na aina ya wasanii anaoshirikiana nao ambao wengi wao wana nguvu ya ushawishi na wanaweza kutengeneza muziki unaokubalika na mashabiki.

Mathalani si ajabu kuona video za nyimbo zake zote ambazo zimetazamwa zaidi ya mara milioni 10 katika mtandao wa YouTube ni zile alizoshiriana na wasanii wengine, yaani kolabo.

Wasanii hao ni Ben Pol (Muziki), Harmonize (Mazoea), Sho Madjozi (I Like It), Mbosso (Looking For You), Alikiba (Proud of You), Nandy & Marioo (Loyalty) na Bien (Nobody).  
Je, kolabo hizi zimefanya nini kwa Darassa na tasnia kwa ujumla?, tunaenda kuangazia baadhi ya hizo kama ifuatavyo.

Hadi sasa video ya wimbo, Muziki (2016) bado inashikilia rekodi kama video ya msanii wa rap Bongo iliyofanya vizuri zaidi YouTube ikitazamwa mara milioni 33, huku ikifuatiwa na ya AY, Zigo Remix (2016).

Kolabo yake na Bien wa kundi la Sauti Sol, Nobody (2023), umesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 17.7 Boomplay na ndio wimbo wa kwanza wa rapa huyo kufikia namba hizo hadi sasa.  

Tukija kolabo yake na Mbosso, Looking For Love (2025), ndio wimbo uliopokelewa vizuri zaidi kutokea katika albamu yake ya pili ‘Take Away The Pain’ iliyotoka chini ya CMG ikiwa na nyimbo 15.

Video yake ilitoka Februari 14 chini ya Mjukuu Visuals, na tayari imetazamwa mara milioni 15 huko YouTube, na ilishika nafasi ya sita katika orodha ya video za Bongofleva zilizofanya vizuri zaidi 2025.

Kwa mara ya kwanza Darassa anashinda Tuzo za Muziki (TMA), ni kupitia kolabo yake na Nandy na Marioo, Loyalty (2020) ambayo ilishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana 2021.

Na wimbo wake na Sho Madjozi kutokea Afrika Kusini, I Like It (2020), si tu ulimuongezea namba ukitazamwa mara milioni 16 YouTube, bali ulifungua milango kwa wasanii wengine Bongo.

Ikumbukwe Darassa ndiye msanii wa kwanza Bongo kufanya kazi na Sho Madjozi, kisha ndio wakafuata wengine kama Marioo (Mama Amina), Nandy (Kunjani) na RJ The DJ (Too Much). Hivyo Darassa ni kama aliwaonyesha kitu.  

Akichangia kuhusu ubora wa Darassa kuchagua wasanii wa kufanya nae kazi Asha Mwidini mkazi wa Dar es Salaam, Chanika anasema “Darasa huwa anafanya vizuri sana akishirikisha wasanii wengine. 

“Ukiangalia nyimbo kama zile alizofanya na Harmonize, kuna mvuto wa kipekee unaotokana na mchanganyiko wa sauti. Hiyo huwa inampa nafasi ya kujaribu ladha mpya za muziki, jambo linalofanya nyimbo zake zifanye vizuri.” Anasema Asha.

Naye Neema Jacob mkazi jijini humo anasema hata akiwa pekeyake kwenye wimbo bado Darassa anauwezo mkubwa

“Mimi naona Darasa peke yake ana uwezo mkubwa, lakini anaposhirikiana na wengine ndipo anapong’ara zaidi. Msanii akishirikiana wimbo unakuwa na nguvu zaidi kuliko ule wa msanii mmoja. Ushirikiano humsaidia hata kufikisha ujumbe kwa mashabiki wa pande zote, ndiyo maana nyimbo zake za collabo zinafanya poa,” anasema Neema.

Aidha Sebastian Onyango anasema Darassa akiwa na wasanii wengine kazi zake zinafanya vizuri zaidi kwani kila msanii huwa na ubora wake.

“Kwa mtazamo wangu, Darasa anajua sana kuchagua watu wa kushirikiana nao. Mara nyingi collabo zake zinafanya vizuri kwa sababu kila msanii huleta ubora wake. Nyimbo zake za solo ni nzuri, lakini zile za ushirikiano zinaingia sokoni haraka zaidi na zinabaki kwenye chati kwa muda mrefu, kitu kinachoonyesha wahenga hawakukosea waliposema kidole kimoja hakivunji chawa.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *