Mkuu wa jeshi la Uganda Muhoozi Kainerugaba siku ya Ijumaa Januri 23, amejisifu kuhusu vifo vya wanachama 30 wa upinzani na kukamatwa kwa wafuasi wao 2,000. EU inalaani vurugu zilizokumba uchaguzi wa hivi karibuni nchini Uganda.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Hadi sasa, tumewaua magaidi 30 kutoka NUP” (National Unity Platform, chama cha kiongozi wa upinzani Bobi Wine), mtoto wa rais alitangaza Ijumaa mapema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X. “Tumewakamata zaidi ya majambazi 2,000 ambao Kabobi (jina la analotumia kwa kumwita Bw. Wine) alifikiri angeweza kuwatumia,” Kainerugaba aliongeza. Mkuu wa jeshi, pia mtoto wa rais Yoweri Museveni, anajulikana kwa machapisho yake ya uchochezi kwenye mitandao ya kijamii na hafichi nia yake ya kumrithi baba yake. Mapema wiki hii, alivunja ukimya wake wa tangu kampeni ya uchaguzi ilipoanza, akitangaza kwenye mtandao wa kijamii wa X, nia yake ya kuona Bobi Wine anauawa.

Wiki iliyopita, Yoweri Museveni alishinda muhula wa saba mfululizo wa urais, kulingana na tume ya uchaguzi, baada ya uchaguzi uliokosolewa na waangalizi na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyobainisha kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kwa siku kadhaa na ukandamizaji wa upinzani. Mpinzani mkuu wa Museveni, Bobi Wine (jina halisi Robert Kyagulanyi), mwanamuziki wa zamani wa muziki wa raggamuffin mwenye umri wa miaka 43, alikimbia baada ya vikosi vya usalama kuvamia nyumba yake siku moja baada ya uchaguzi, matokeo yake ambayo aliyashutumu kama “yaliibiwa.”

Umoja wa Ulaya ulielezea wasiwasi wake siku ya Ijumaa, ukilalamikia “ghasia na vitisho vya kabla na baada ya uchaguzi, haswa dhidi ya kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi.” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema siku ya Alhamisi kwamba alikuwa akifuatilia “kwa wasiwasi hali ya baada ya uchaguzi nchini Uganda, ikiwa ni pamoja na ripoti za watu kukamatwa, kuwekwa kizuizini, na matukio ya vurugu yanayowahusisha watu wa upinzani na wafuasi wao.

“Hali inayozidi kukua”

Kulingana na mchambuzi wa siasa, akizungumza na RFI kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama, idadi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi. Lakini anasema hashangai, kwani ukandamizaji hurudiwa kila uchaguzi. “Ni hali inayozidi kukua. Tangu Uganda ilipopitisha Katiba mpya mwaka wa 1995, tumekuwa na mfululizo wa chaguzi za kawaida kila baada ya miaka mitano. Na kila wakati, vurugu zimeongezeka. Kwa hivyo njia iko wazi. Zaidi ya hayo, haswa kwa jamii ya kimataifa, wanaposikia neno ‘uchaguzi,’ wanafikiri ni uchaguzi, yaani, shughuli za kiraia. Ilhali nchini Uganda, uchaguzi ni operesheni ya kijeshi.”

Mtaalamu huyu pia anashangazwa na “jinsi jumuiya ya kimataifa imehusika kwa mbali au kwa karibu katika ukandamizaji unaofanywa.” “Hapo awali, washirika wa maendeleo wa Ulaya walifanya kama aina ya udhibiti wa matumizi mabaya ya utawala. Lakini sasa, nadhani utawala umegundua vyema kwamba nchi hizi zinazingatia zaidi shughuli za biashara za makampuni yao nchini Uganda. Kwa hivyo utawala unaona kwamba unaweza kutekeleza ukandamizaji wake bila mtu yeyote kuzuia kinachoendelea.” “

Siku ya Alhamisi Januari 22, polisi ya Uganda pia ilitangaza kukamatwa kwa Mbunge wa NUP Muwanga Kivumbi, ambaye aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wafuasi 10 waliuawa na jeshi ndani ya nyumba yake huko Butambala (katikati mwa Uganda) usiku wa uchaguzi. Kulingana na vyombo vya usalama, kukamatwa kwa watu hao “kunahusishwa na matukio ya hivi karibuni ya vurugu za kisiasa huko Butambala.”

Waganda zaidi ya 600 wamekamatwa kwa kuandamana kupinga ushindi wa Yoweri Museveni, wakili wa upinzani Erias Lukwago pia alisema siku ya Jumatano. “Wateja wetu wanakana mashtaka yote. Baadhi wanadai walikamatwa majumbani mwao na polisi na kuzuiliwa kabla ya kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ambayo hawajui chochote kuhusiana nayo,” Lukwago ameliambia shirika la habari la AFP.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *