Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeanza mkakati wa kubaini walipakodi wanaoficha taarifa zao nje ya nchi kwa lengo la kukwepa kodi.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja baina ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda na wakaguzi kutoka Global Forrum wakiongozwa na Mshauri wa Sera za Kodi, Puneet Gulati kuhusu uwazi na kubadilishana taarifa za kodi.
Mwenda amesema kwa kujiunga na mfumo wa kubadilishana taarifa za kimataifa kutaongeza uwazi na kusaidia TRA kubana kampuni kubwa zinazoficha taarifa zake nje ya nchi ili kukwepa kodi na kuokoa mapato.
Amesema kwa sasa TRA itatengeneza mfumo wa kodi utakaowezesha kila mmoja kulipa kodi inayostahili kwa walipakodi wa ndani na wa nje ya nchi na kuleta usawa ili kuongeza makusanyo ya kodi na kuimarisha uchumi.
Awali Kamishna wa walipakodi wakubwa, Michael Muhoja amesema wanataka kila mmoja alipe kodi kule alikopatia hela kwa kufuatilia taarifa zake na TRA itakapoingia katika utaratibu huo itaweza kukusanya kodi zaidi na kuleta usawa.
Mshauri wa Sera za Kodi kutoka Global Forrum, Puneet Gulati amesema anatarajia Tanzania itaendelea kupiga hatua kwa kufuata miongozo na mapendekezo yaliyotolewa ili kukidhi vigezo vya kupata taarifa za kimataifa moja kwa moja.
Timu hiyo ya wakaguzi imekuwepo nchini kukutana na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na binafsi kutoka Tanzania Bara pamoja na Zanzibar ambazo ni wadau muhimu wa utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya ubadilishanaji wa taarifa za kodi.
#StaeTvUpdate
(Feed generated with FetchRSS)