Benfica, Ureno. Mashabiki lialia wa Benfica wamevamia uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wakitaka majibu kuhusu kiwango duni cha timu yao chini ya Kocha Jose Mourinho aliyeteuliwa Septemba mwaka jana baada ya kuachana na  Fenerbahce.

Hata hivyo, uwepo wa kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United, hauonekani kukidhi malengo ya mashabiki waliyokuwa nayo wakati anajiunga nao.

Benfica kwa sasa haijapoteza mchezo wowote katika ligi ya Ureno, lakini inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na tofauti ya pointi 10 nyuma ya vinara FC Porto.

Pia wapo kwenye hatari kubwa ya kukosa nafasi ya kucheza hatua ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hadi sasa wameshatolewa kwenye Kombe la Ureno katika hatua ya robo fainali. Hali hiyo imewafanya mashabiki kuamua kuchukua hatua wenyewe.

Kwa mujibu wa gazeti la Ureno, Correio da Manha, kundi la mashabiki wapatao 200 walivamia uwanja wa mazoezi wa klabu uliopo Seixal wakidai kuzungumza na viongozi wa klabu akiwemo Mourinho, mkurugenzi wa ufundi Simao Sabrosa na nahodha Nicolas Otamendi.

Awali, wanachama wanne wa kundi hilo waliruhusiwa kuingia kabla ya wengine pia kudai nao waruhusiwe. Polisi waliitwa kudhibiti hali hiyo, lakini waliwaruhusu mashabiki kuingia baada ya kudai wangefanya maandamano kwa amani.

Mashabiki hao walizungumza na Mourinho, Simao na Otamendi kwenye moja ya viwanja vya mazoezi na kuondoka baada ya saa moja. Rais wa klabu, Rui Costa, tayari ametoa msimamo wake kuhusu hali ya sasa.

Alipoulizwa kama klabu inaweza kuamua kuachana na Mourinho, alijibu:

“Hapana. Yeye ni kocha bora na tayari amethibitisha hilo. Si msimu mwepesi. Kumfukuza kocha? Hilo halipo kabisa.”

Alipoulizwa kama klabu inaweza kufanya usajili zaidi, Costa aliongeza:

“Siwezi kuahidi chochote, lakini tutaona hadi mwisho wa dirisha la usajili itakavyokuwa. Tutapambana hadi sekunde ya mwisho kufikia malengo yetu. Bado kuna ubingwa wa kupigania.”

Benfica ilirejea dimbani Jumapili kupambana na Estrela da Amadora katika mchezo wa ligi, kabla ya kuendelea na kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya klabu ya zamani ya Mourinho, Real Madrid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *