Taarifa ya tume hiyo imeonya kuwa pia taarifa za kuhamasishwa kwa majeshi katika Jimbo la Jonglei inaongeza kwa kiwango kikubwa hatari ya machafuko ya halaiki dhidi ya raia na kudhoofisha zaidi makubaliano dhaifu ya amani ya nchi hiyo.

Tume imesema hali hii inajitokeza wakati misingi ya kisiasa ya mchakato wa amani tayari imeyumba kwa kiasi kikubbwa.

Uchochezi kutoka kwa walio madarakani

Kwa mujibu wa Tume, kauli zinazotolewa hadharani za makamanda na wengine wenye mamlaka ya amri na udhibiti, zinapochanganywa na uhamasishaji hai wa vikosi, ni ishara hatari chini ya sheria za kimataifa.

“Lugha inayotaka kuuawa kwa wale walio nje ya mapigano na raia, wakiwemo wazee kwa madai kwamba hakuna anayepaswa kuokolewa si ya kushtua tu, bali ni hatari kubwa,” amesema Yasmin Sooka, Mwenyekiti wa Tume, akisisitiza kuwa kauli hizo zinaweza kuondoa matarajio yoyote ya kujizuia kwa askari walioko uwanjani.

Cha kujifunza kutoka historia ya vurugu

Sooka ameonya kuwa historia ya Sudan Kusini inaonesha jinsi maneno yanavyoweza kubadilika haraka na kuwa umwagaji damu.

“Katika siku za nyuma Sudan Kusini,kauli kama hizo zimekuwa zikitangulia mauaji ya halaiki,” amesema akiongeza kuwa “Zinapotolewa au kuvumiliwa na walio katika nafasi za uongozi, zinatoa ruhusa ya kufanya vurugu na kuiweka jamii nzima katika hatari kubwa, hasa wakati ambapo raia tayari wamekimbia makazi yao, wameathirika kisaikolojia na wako hatarini”.

Uwajibikaji wa uongozi na athari za kisheria

Tume imesisitiza kuwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na jinai, viongozi wa kijeshi na wa kiraia wanaweza kuwajibishwa binafsi si tu kwa uhalifu wanaoamuru au kutekeleza, bali pia kwa uhalifu wanaouchochea au kushindwa kuuzuia.

Kamishna Carlos Castresana Fernández amesema kuwa kauli za hadharani zinazohamasisha mashambulizi dhidi ya raia, au kuwasilisha jamii nzima kama walengwa halali, “zinaweza kusababisha uwajibikaji wa jinai wa mtu binafsi,” akibainisha kuwa uwajibikaji wa amri unatumika hata pale maagizo yanapotolewa kupitia vitisho vya hadharani au uvumilivu wa makusudi wa uchochezi.

Wito wa haraka wa kuchukua hatua

Akielezea hali ya sasa kama “wakati wa hatari kubwa na wajibu wa kisiasa,” Kamishna Barney Afako ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kuwadhibiti wanajeshi, kupunguza mvutano na kurejesha nidhamu.

“Bila kuingilia kati kwa kiwango cha juu kabisa, Sudan Kusini iko hatarini kuteleza kwa kasi kuelekea awamu nyingine ya vurugu zilizosambaa,” ameonya, akiongeza kuwa ushiriki wa haraka wa kikanda sasa unahitajika ili kuokoa makubaliano ya amani. “Muda unatutupa mkono.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *