Katika ujumbe wake mahsusi kwa sikuu Guterres amesema sayansi inaonesha dunia kwa muda sasa inaelekea kuvuka kiwango muhimu cha ongezeko la joto duniani la nyuzi 1.5C. Wajibu uliopo sasa ni kuhakikisha uvukaji huo unakuwa “mdogo kadri iwezekanavyo, wa muda mfupi, na salama kwa kuharakisha mpito wa haki, uliopangwa na wenye usawa kutoka kwenye nishati ya mafuta ya kisukuku. Na Kiini cha mpito huo ni nishati safi au jadidifu”.

Mvuvi wa Kenya amesimama katika mashua ndogo ya mbao iliyojaa mitego ya uvuvi.

Wavuvi wa Kenya Wanasafiri Kwenye Maji ya Pwani kwa Msaada wa FAO

Nishati mbadala yakumbatiwa na jamii ya wavuvi Kwale nchini Kenya

Nchini Kenya, mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kuhakikisha uzalishaji wa nishati mbadala unaongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2030 unazidi kushika kasi kwani hivi sasa hata wavuvi na wamiliki wa migahawa wameanza kutumia majokofu yanayotumia nishati ya sola kuhifadhi samaki, na hivyo kuwa na sio tu uhakika wa samaki wakati wote bali pia wachuuzi kuepukana na kitoweo hicho kuoza umeme unapokatika. Assumpta Massoi anatupatia simulizi hiyo ya mafanikio kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati endelevu, IRENA.

Video inaanzia ufukwe wa Diani kwenye kaunti ya Kwale nchini Kenya. Hapa ni eneo la jamii ya wavuvi na umsikiaye ni Shee Lanjoro, Meneja wa mgahawa wa Mvureni ulioko hapa pwani. Anasema sasa tunaelekea msimu wa vimbunga. Ghafla bahari itachafuka na wavuvi hawatoweza kwenda kuvua. Kwa hiyo chochote tunachoweza kuvua sasa tunahitaji kuhifadhi kwa miezi miwili ijayo.

Ingawa hivyo wana changamoto.

“Lengo letu kuu ni kuendeleza hii jamii ya wavuvi ambao ndio wanamiliki eneo hili. Tunajaribu kununua samaki kutoka kwao kwa bei ya juu kuliko ile ambayo wangepata iwapo wangeuza kwenye soko la hapa. Bila shaka kama wafanyabiashara tuna changamoto chache na kubwa kuliko zote ni jinsi ya kuhifadhi samaki tunaonunua.”

Felix Lusaka ni fundi wa sola na muuzaji wa nishati mbadala anasema,

“Tatizo wanalokabiliana nalo watu hapa ni kukatika mara kwa mara kwa  umeme wa gridi ya taifa kutoka shirika la Umeme la Kenya,(KPLC), na wakati huo huo tuna watu walio maeneo ya mbali zaidi ambao hawapati umeme huu, mfano walioko ufukweni.”

Mwanasha Mwachalika mchuuzi wa samaki akiwa dukani mwake anasema changamoto kubwa ni umeme kukatika wakati mwingine kwa saa mbili hadi tatu. Akisema stima anamaanisha umeme…

Hakika sola zimefungwa juu ya paa za nyumba na Meneja wa mgahawa Bwana Lanjoro anasema..

Kwa sasa tumefunga paneli tatu. Kama kuna njia ya kujitoa kwenye gridi ya taifa ya umeme ni kutegemea nishati safi. Nadhani hii ndio njia. Mosi ni nafuu, pili ni nzuri kwa mazingira, na tatu, bila shaka itapatikana wakati wowote kwa kutambua kuwa tuko juu ya Ikweta ambako tuna jua nyakati zote. Kwa hiyo nishati safi ndio jawabu.”

Kwa fundi wa sola Lusaka… sola haiijatupatia tu mwanga bali pia imetupatia mustakabali.

Jeremiah Mutungi, mmoja wa wavuvi hapa Diani anatamatisha kwa ushuhuda.

“Niliingia katika jamii ya wavuvi, nikavua samaki. Lakini kwa wakati huu nashukuru Mungu tumepata sola na samaki wetu tunawakausha kwa kutumia sola, na tunaona tunaendelea vizuri.”

Kuongeza mara tatu uzalishaji wa nishati mbadala ifikapo mwaka 2030 ni jukumu muhimu katika kupunguza kwa haraka na kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi duniani, ili kuhakikisha ongezeko la joto duniani halivuki nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi, moja ya makubaliano ya mkutano wa COP28 uliofanyika Dubai, Falme za kiarabu.

Kikundi cha wajasiriamali nchini Rwanda na viongozi wa Afrika wenye tabasamu wakipiga picha kwenye hafla ya FAO iliyozingatia mabadiliko ya mfumo wa kilimo na vyakula barani Afrika.

Washiriki wa tukio la FAO wanasherehekea uongozi wa kilimo na chakula barani Afrika.

Mradi wa HASTEN unaoendeshwa na  FAO waleta tija kwa vijana na wanawake Rwanda

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula  na kilimo Duniani FAO, kupitia mradi wake wa masuala ya biashara HASTEN limeendesha warsha maalum ya kuanzisha biashara kwa vijana na wanawake,  mjini Kigali Rwanda, lengo likiwa ni kuwapa miradi 10 mipya ya biashara itakayofanyika kwa msaada maalum kutoka kwa wakufunzi wa kitaifa na kimataifa juu ya mbinu za kupanua biashara, kuongeza ufanisi na kuchangia katika malengo ya maendeleo endelevu SDGs. Sheilah Jepngetichn ana taarifa zaidi,

Dhumuni kuu la mradi wa HASTEN uliojikita katika sekta ya kilimo ni kujenga ujuzi wa kufikiria kwa mfumo, kusaidia biashara zinazojumuisha masuala ya kiikolojia na kijamii, na kuunganisha serikali, vyuo na sekta binafsi ili kuharakisha mabadiliko ya mifumo ya chakula na kilimo. Warsha hii ya FAO inalenga biashara ndogo na za kati (MSMEs) zinazoongozwa na vijana na wanawake, ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kuimarisha ukuaji wa miradi yao. Ozonio Ojielo, ambaye ni  mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda, anasema

“Tunahitaji kuimarisha msaada kwa vijana na wanawake kwa sababu wao ndio mustakabali wa sekta hii. Kuongeza uwekezaji katika kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi na ubunifu unaojumuisha jamii ndilo hatua ya kuwapa nguvu vijana na wanawake kuchangia kwenye kulinda mazingira na mnepo dhidi ya tabianchi, na kufanikisha maono yetu ya 2050.”

Hajnalka Petrics ni Afisa wa malengo ya maendeleo endelevu wa FAO, anasema,

Kuona shauku na kujitolea kwa wajasiriamali hawa ni kitu cha kuhamasisha. Kupitia HASTEN, wanajifunza si tu jinsi ya kuboresha biashara zao na maandalizi ya kifedha, bali pia jinsi ya kupima na kufuatilia athari zao kijamii na kimazingira. Hii inawaandaa kuwa viongozi wa kweli wa mabadiliko na kuharakisha maendeleo kuelekea SDGs.

Vijana na wanawake wanapata ujasiri na ujuzi kupitia warsha ya FAO HASTEN Kigali. Miongoni mwa washiriki wa warsha, hii ni Tifare Kaseke wa Erthwise Storage, anafunguka,

“Awali nilikuwa na wasiwasi kuhusiana na biashara, lakini baada ya warsha hii na msaada wa wakufunzi, sasa ninajiamini zaidi kuzungumza na wawekezaji, na nimejifunza jinsi ya kujenga mahusiano na watu wapya na kukuza ujuzi wangu binafsi.”

Warsha hii imeonesha jinsi vijana na wanawake wanaweza kufanya mabadiliko endelevu katika mifumo ya chakula na kilimo Rwanda, huku wakiimarisha biashara zao na kuchangia maendeleo ya kijamii na kimazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *