Dodoma. Serikali imeagiza kila Mtanzania kuweka nadhiri ya kupanda walau mti mmoja kwani, baada ya miaka 10 Tanzania itakuwa imepanda miti zaidi ya bilioni 61 ambacho ni kiwango kikubwa.

Wito huo umetolewa leo Jumanne Januari 27, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Dk Festo Dugange alipoongoza shughuli ya kupanda miti kwenye mji wa Kiserikali Mtumba.

Dk Dugange amesema kwa sasa Watanzania wapo takribani milioni 61 ambapo kila mmoja akilazimika kupanda mti mmoja kwa mwaka inaweza kupandwa miti mingi kwa wakati mmoja.

“Lakini kupanda ni kitu kimoja na kutunza ni kitu kingine, tuwe na tabia ya kutunza miti siyo kupanda na kuacha mwisho wake tunakosa matokeo ya tunachokilenga kama nchi,” amesema Dk Dugange.

Naibu Waziri amesimamia upandaji miti katika eneo hilo kwa watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na wananchi na jumla ya miti 693 imepandwa katika eneo lililozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipokuwa Makamu wa Rais 2017.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinaonyesha Tanzania inapoteza ekari 150,433 za miti ambazo zinakatwa kwa ajili ya matumizi ya mkaa na inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 inaweza kupoteza ekari 2.8 milioni kutokana na ongezeko la watu.

Amesisitiza upandaji wa miti utakuwa endelevu kwani maeneo ya kupanda miti bado yapo na miti inapatikana kwa urahisi.

Awali, Kamishina wa uhifadhi kutoka TFS, Dk Zainabu Bungwa amesema matumizi ya shughuli za binadamu ndiyo chanzo cha uharibifu mkubwa wa mazingira na hata kutishia jangwa.

Naibu Waziri Dk Festo Dugange akipanda mti eneo la mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Dk Bungwa amesema binadamu hao hao wanaweza kuzuia jangwa kama wataamua kupanda miti na kuona umuhimu wa utunzaji wa misitu kama chanzo cha mvua, dawa, matunda, vivuli na vyanzo vya maji.

Amesema hadi sasa Tanzania ina jumla ya misitu 465 ambayo inamilikiwa na Serikali Kuu, serikali za mitaa, vijijini na mamlaka zingine na kati ya hiyo, 26 ni hifadhi za misitu ya asili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *