“Nilichopitia ni mtihani mkubwa, lakini huku uhamishoni nimepata nguvu kubwa kuliko silaha yoyote ya kivita,” anasimulia Nafeesa, ambaye sasa anaanza kujenga upya maisha yake kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
“Mume wangu, walimuua kule Nyala (Darfur). Walitujia saa saba na nusu usiku, mnamo tarehe 2 Agosti 2023. Walikuja usiku… Alipoinuka kitandani, walimpiga risasi tatu. Mimi nilifungwa kamba, na pia walimfunga mwanangu aliyekuwa na umri wa miaka tisa. Walichukua pesa zetu, mali zetu na nguo kwa magari yao.”
“Mama yangu alisema hatuwezi kuishi pale tena. Tukaja Am Dafok, kisha nikaondoka Am Dafok kwenda Birao. Shirika la UNHCR lilitupokea, namshukuru Mungu. Walinipa nafasi hii hapa na walinipa nyumba. Walitupatia mablanketi na magodoro kwa ajili ya watoto wangu. Ninashukuru kwamba walinipa nyumba ninamoishi sasa.”
Majora Sifamwelwa Akalaluka, ambaye anaongoza juhudi za kushirikiana na jamii za MINUSCA huko Birao, anazungumza na wanawake kwenye soko la miji.
Usalama katika eneo hilo la mpaka unaimarishwa na walinzi wa amani wa MINUSCA, ambao hufanya doria mara kwa mara ili kuzuia machafuko na kuhakikisha kuwa wakimbizi na wenyeji wanaishi kwa utulivu.
Mshirika wa Ulinzi katika Jamii, wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), Jofroy Fabrice Sanguebe-Nadji anaeleza kuwa wakimbizi wengi ni wanawake na Watoto waliolazimika kukimbia ukatili ili kutafuta hifadhi.
“Leo, tuna idadi ya wakimbizi wa Sudan wasiopungua 27,000, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kufuatia mapigano kati ya Majeshi ya Sudan na Kikosi cha Rapid Support Forces. Walilazimika kukimbia ukatili na mzozo wa silaha ili kupata hifadhi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.”
“Uwepo wa MINUSCA ni rasilimali kubwa. MINUSCA imekuwa na jukumu kuu katika utekelezaji wa mamlaka ya ulinzi wa kimataifa ya UNHCR. Uwepo wao unasaidia kuhakikisha kiwango cha chini cha usalama, kuruhusu wafanyakazi wa UNHCR na washirika wao kufanya kazi kwa uhuru mjini Birao na kwenye njia zinazozunguka.”
Meja Obed Mumba, Kamanda wa Kikosi Kazi cha MINUSCA huko Am Dafock akiwa mpakani anaelezea namna hali ya ulinzi na usalama inavyoendelea kuimarika.
(Akizungumza na mwenzake): “Kila kitu kiko sawa?” (Jibu): “Kila kitu kiko sawa.”
(Akiendelea kuelezea): “Tuko karibu kabisa na mpaka. Upande huu ni Sudan na upande huu ni Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wasudan na watu wa Afrika ya Kati walikubaliana jinsi ambavyo wangekuwa wakifanya kazi na jinsi ambavyo wangekuwa wakitembea. Watu sasa wako huru kutembea kutoka Sudan kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati.”
“Kama MINUSCA, tumeendelea kutekeleza mamlaka yetu ya ulinzi wa raia na tunahakikisha kuwa kila kunapokuwa na tatizo, tunafika haraka na kuwasaidia.”
Mwanamke mkimbizi wa Sudan anamfundisha mwanamume jinsi ya kufanya kazi shambani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ili wote waweze kujikwamue kimaisha.
Nguvu ya mama katikati ya vita
Nafeesa anasimulia kile ambacho amevumilia na jinsi, akiwa uhamishoni, alipata nguvu yenye uwezo zaidi kuliko silaha yoyote ya vita.
Nafeesa (Akieleza kuanza maisha mapya):
“Naamka na watoto wangu asubuhi. Nawaandalia chai na kifungua kinywa. Nilikuja hapa kufanya kazi. Natumia siku nzima nikifanya kazi. Nauza vitu vidogo ili kupata pesa ya matumizi yangu.”
“Wanaweza kuchukua vitu kutoka nyumbani kwako. Wanaweza kumchukua mumeo kutoka kwako, kama mimi nilivyompoteza wa kwangu. Na watoto wanaweza kuwa wahanga. Lakini sasa nimekuja hapa, namshukuru Mungu.”
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kuongeza muda wa kuhudumu kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Udhibiti wa Hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) hadi tarehe 15 Novemba 2026. Hatua hii inakuja wakati ujumbe huo ukizidi kuwa na jukumu muhimu katika kulinda raia na kusaidia wakimbizi wanaokimbia mizozo katika nchi jirani.
Katika azimio lake, Baraza la Usalama limeagiza MINUSCA kutoa kipaumbele katika ulinzi wa raia dhidi ya vitisho vya vurugu, kusaidia upanuzi wa mamlaka ya serikali nchi nzima, na kuandaa mazingira salama kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2025 na 2026.
Upanuzi wa mamlaka ya MINUSCA unatazamwa kama nguzo muhimu ya utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na ukanda mzima wa Afrika ya Kati, hususan katika kipindi hiki ambacho mataifa jirani kama Sudan yanakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama.