
Yanga inaikaribisha Dodoma Jiji FC katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaoanza saa 1:00 usiku.
Ushindi wa leo utaifanya Yanga ifikishe pointi 22 na hivyo kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi wakati kwa Dodoma Jiji, ushindi utawafanya wawe na pointi 13 na watasogea hadi nafasi ya nane.
Wakati timu hizo zikijiandaa kukutana katika mchezo wa 11 kwenye Ligi Kuu baina yao, wageni Dodoma Jiji mbali na kupata pointi tatu tu muhimu, mchezo wa leo ni fursa kwao kumaliza unyonge walionao dhidi ya Yanga tangu waliposhiriki kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu msimu wa 2021/2022.
Katika historia, Yanga imeibuka na ushindi mara tisa kati ya mechi 10 iliyocheza na Dodoma Jiji kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara huku mechi moja ikimalizika kwa sare.
Ubabe wa Yanga dhidi ya Dodoma Jiji haujaishia katika ushindi tu bali hata takwimu za ufungaji na ulinzi katika mechi baina yao. Kwenye mechi hizo 10 ambazo zimekutanisha timu hizo mbili, Yanga imefunga mabao 29 sawa na wastani wa mabao 2.9 kwa mchezo huku Dodoma Jiji ikifunga mabao matatu tu.
Ushindi mkubwa ambao Yanga imeupata dhidi ya Dodoma Jiji ni kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita ambapo ilipata ushindi wa mabao 5-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi amesema kuwa ukubwa wa kikosi chao utakuwa chachu ya ushindi dhidi ya Dodoma Jiji.
“Tumepata muda mdogo wa maandalizi ya mchezo wetu wa kesho baada ya mchezo wetu wa ugenini dhidi ya Al Ahly na safari ndefu. Lakini tuna kikosi kipana na hatuna budi kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wetu.
“Wote kwa pamoja tunajua umuhimu wa mchezo wetu wa kesho na matokeo ya mchezo wetu uliopita hayawezi kutuadhiri na mipango yetu. Wachezaji wote kwa asilimia kubwa wako sawa kiafya na wapo tayari kupambana,”
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Amani Josiah amesema kuwa wamejipanga kwa ajili ya mchezo huo.
“Tunacheza mechi kubwa na dhidi ya timu kubwa. Jukumu letu kubwa kama benchi la ufundi ni kuwaweka wachezaji kuwa wenye utayari na mchezo.
“Tuna wachezaji wenye uzoefu wa kuicheza na kuifikiria mechi hiyo. Nadhani tupo tayari na tumeshafanya maandalizi,” amesema Josiah.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo utakuwa baina ya Coastal Union na KMC katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuanzia saa 3:00 usiku.