
Kwa muujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, ombi la msaada wa kibinadamu kwa ajili ya Somalia kwa mwaka 2026 liko chini kwa asilimia 40 ikilinganishwa na ombi la mwaka jana na linalenga kusaidia watu milioni 2.4, chini ya nusu ya watu wote wanaohitaji msaada wa kibinadamu.
“Mpango huu umeundwa kusaidia chini ya nusu ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu,” amesema, akisisitiza kuwa kupungua kwa lengo hilo kunatokana na uhaba wa fedha, si kuboreka kwa hali halisi nchini humo.
Ukata wa ufadhili ni mtihani mkubwa
“Upungufu huu unatokana na rasilimali chache si kwa sababu mahitaji ya kibinadamu yamepungua,” Dujarric amewaambia waandishi wa habari jijini New York, akisisitiza kuwa Somalia inaendelea kukabiliwa na migogoro inayofuatana inayochochewa na mishtuko ya tabianchi, migogoro ya kivita na changamoto za kiuchumi.
Ameyonya kuwa bila msaada wa haraka na ulioongezwa kwa kiwango kikubwa, hali inaweza kuzorota kwa kasi.
“Bila msaada wa dharura na ulioongezwa, mchanganyiko wa ukame wa muda mrefu, kuporomoka kwa vyanzo vya kipato, watu kukimbia makazi yao, milipuko ya magonjwa na kupungua kwa misaada ya kibinadamu kutaongeza uhaba wa chakula, uhaba wa maji, na hatari za kiafya zitaongezeka,” amesema.
Dujarric amerejelea pengo la ufadhili la mwaka jana kama onyo la wazi la kile kinachoweza kutokea.
“Mwaka 2025, Mpango wa Hatua za Misaada ulifadhiliwa kwa asilimia 27 pekee ni dola milioni 397 tu kati ya dola bilioni 1.4 tulizoomba,” amesema, akibainisha kuwa upungufu huo uliyalazimu mashirika ya kibinadamu “kupunguza kwa kiasi kikubwa, na katika baadhi ya matukio kusitisha kabisa, misaada ya kuokoa maisha ya binadamu.”
Umoja wa Mataifa umewataka wafadhili kuchukua hatua za haraka, ukionya kuwa kuendelea kwa ufadhili duni kunaweza kusukuma jamii zilizo tayari dhaifu katika mgogoro mkubwa zaidi, huku mateso yanayoweza kuzuilika na vifo vikiongezeka.