
Dar es Salaam. Mji wa Katoro mkoani Geita unaendelea kujijenga kama kitovu kipya cha biashara nchini, ukitambulika kwa nafasi yake ya kimkakati katika mtiririko wa bidhaa na huduma si tu kwa Tanzania, bali pia kwa kanda ya Afrika Mashariki na nchi jirani.
Kadri sekta ya biashara inavyoelekeza macho yake katika miji midogo yenye fursa kubwa za masoko na uwekezaji, Katoro imeibuka kama eneo lenye umuhimu wa kipekee katika kuunganisha wafanyabiashara na wanunuzi kutoka miji na vijiji vinavyoizunguka.
Katika jitihada za kuimarisha nafasi hiyo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeanza kuwekeza katika tafiti maalumu za masoko na uchambuzi wa fursa za kibiashara Katoro. Tafiti hizo zinalenga kupanua masoko, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinapata nafasi thabiti katika biashara ya kikanda na kimataifa.
Matokeo ya awali ya tafiti hizo yanaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya bidhaa zinazouzwa Katoro zinatoka nje ya nchi, hali inayoonesha fursa kubwa iliyopo ya kuhimiza uzalishaji wa ndani, kuongeza ushindani na kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.
Mpango huo ulielezwa Januari 26, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk Latifa Khamis, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara katika ofisi za taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
“Katoro ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za biashara kutokana na ukaribu wake na nchi jirani pamoja na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na biashara,” amesema Dk Latifa.
Amesema TanTrade iko tayari kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara katika kutekeleza maono ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha biashara zinakua na bidhaa pamoja na huduma za Tanzania zinapata masoko ya uhakika ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.
Kwa mujibu wa Dk Latifa, TanTrade imejipanga kimkakati kwa kuimarisha uwepo wake katika maeneo muhimu ya biashara, ikiwa na ofisi Makao Makuu Dar es Salaam pamoja na ofisi za kikanda Dodoma, Mwanza na Arusha.
Aidha, amesema taasisi hiyo ina mpango wa kufungua ofisi katika maeneo ya mipakani ikiwemo Kigoma na Songwe (Tunduma), hatua inayolenga kuimarisha huduma za intelijensia ya masoko na kuongeza fursa za biashara kwa wadau.
“Kuwepo kwetu Katoro kutarahisisha upatikanaji wa taarifa za masoko, kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa eneo hilo na kuwasaidia kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema.
Amefafanua kuwa majukumu ya TanTrade ni pamoja na kufanya tafiti na intelijensia ya masoko, kutoa taarifa za masoko na bei, kujenga uwezo wa wafanyabiashara, kuratibu matukio ya kukuza biashara, pamoja na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya biashara.
Kwa mujibu wa Dk Latifa, hadi sasa TanTrade imefanikiwa kuyaunganisha zaidi ya makampuni 1,065 ya Kitanzania na masoko ya nje, huku vijana na wanawake 14,045 wakinufaika na mafunzo ya ujasiriamali na biashara shindani.
Ameongeza kuwa kupitia maonesho ya kimataifa, TanTrade imeratibu na kufanikisha upatikanaji wa mikataba 36 yenye thamani ya Sh17.35 trilioni katika Expo 2020 Dubai, mikataba mingine minane yenye thamani ya Sh38 bilioni kupitia maonesho ya Osaka nchini Japan, pamoja na mikataba 10 yenye thamani ya zaidi ya Sh176 bilioni iliyosainiwa katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam mwaka jana.
Katika hatua nyingine, amesema TanTrade imefanikisha kuanzishwa kwa nembo ya taifa ya ‘Made in Tanzania’, inayolenga kutambulisha, kulinda na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
“TanTrade itaendelea kupanua wigo wa masoko, kuimarisha tafiti za biashara na kusogeza huduma zake karibu zaidi na wafanyabiashara, hususan katika miji ya kimkakati kama Katoro,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema maamuzi yanayofanywa sasa katika sekta ya biashara na viwanda yataamua mustakabali wa Tanzania kwa vizazi vijavyo.
Amesema dunia ya sasa ina ushindani mkali wa kiuchumi, hivyo Tanzania haina budi kujipanga kikamilifu ili kulinda maslahi yake na kuamua hatima yake yenyewe.
“Dunia haina huruma. Ni mazingira ya ushindani ambako mwenye nguvu ndiye anayesimama. Hatima ya Tanzania lazima ibaki mikononi mwa Watanzania,” amesema Londo.
Ameeleza kuwa biashara ni mhimili mkuu wa maendeleo kwa kuwa ndiyo chanzo cha ajira, utulivu wa kijamii na ukuaji wa uchumi, akisisitiza kuwa maamuzi ya sasa yanapaswa kulenga kuifanya Tanzania kuwa mahali salama na rafiki kwa kuishi na kufanya biashara, si Dar es Salaam pekee bali hata katika miji inayokua kama Katoro.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Londo amesema itaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi iwapo wakulima wataondolewa kwenye uzalishaji wa mazao ghafi na kuunganishwa katika minyororo ya thamani ya bidhaa.
“Kumfikisha mkulima kwenye mnyororo wa thamani kunahitaji tafiti za kina, intelijensia ya masoko na ushauri wa kitaalamu. Hapa ndipo jukumu la TanTrade linapokuwa muhimu,” amesema.
Ameongeza kuwa TanTrade ina wajibu wa kuishauri Serikali katika kuunda na kusimamia sera na mikakati ya biashara ili kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinapata utambulisho wa kibiashara unaotambulika kimataifa na kuuzwa kwa bei ya haki.
Kwa mujibu wa Londo, utambulisho wa kibiashara wa taifa ni nguzo muhimu ya ushindani wa kimataifa, akibainisha kuwa nchi nyingi hutumia fedha nyingi kujenga taswira na hadhi ya bidhaa na huduma zao ili kuongeza thamani katika masoko ya dunia.
“Bila utambulisho wa kibiashara, bidhaa zetu zinaweza kuuzwa, lakini wazalishaji wetu hawapati faida stahiki,” amesema.
Amesema Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini mifumo ya biashara ya dunia haiwapi fursa nchi zinazoendelea kunufaika ipasavyo bila mikakati madhubuti, hivyo matumizi ya tafiti na intelijensia ya masoko ni jambo lisiloepukika.
“Serikali itaendelea kuimarisha taasisi zake za biashara, hususan TanTrade, ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania, kujenga uwezo wa wafanyabiashara na kufikisha fursa hizo hadi katika miji inayokua kwa lengo la kuhakikisha taifa linanufaika kikamilifu na rasilimali zake,” amesema Londo.