
Dodoma. Tukio la maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, mwaka jana, limeendelea kuwa mjadala kwa wadau mbalimbali na sasa limefika bungeni, ingawa wamelijadili kwa mtindo wa sitaki nataka.
Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walihoji undani wa yaliyotokea, huku wengine wakiishia kutoa pole kwa Watanzania walioathiriwa na matokeo ya vurugu hizo.
Oktoba 29, mwaka jana siku ya uchaguzi mkuu, kuliibuka maandamano yaliyozaa vurugu katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.
Hata hivyo, katika hotuba yake ya kulizindua Bunge la 13, Novemba 14, mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alionesha kusikitishwa na kilichotokea huku akiahidi kuunda tume kuchunguza kiini cha tatizo.
Novemba 19, mwaka jana, mkuu huyo wa nchi aliiunde tume hiyo na tayari imeshaanza kukutana na makundi mbalimbali wakiwamo waathirika wa vurugu hizo.
Mjadala kuhusu tukio hilo, umeibuka bungeni jijini Dodoma leo, Januari 27, 2026 katika kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Bunge la 13, wakati wabunge walipokuwa wanachangia hotuba ya Rais Samia ya siku ya kulizindua Bunge hilo.
Miongoni mwa wabunge walioibua mjadala huo ni wa Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava aliyesema ni vema wabunge wakapata nafasi ya kujadili jambo lililotokea Oktoba 29, kwa kuwa, nje ya Bunge kuna maoni mengi yanayotolewa.
“Ni vizuri tupate nafasi ya kujadili jambo hili lililotokea Oktoba 29, huko nje yako maoni mengi kuhusu tume inayochunguza jambo hili.
“Nchi yetu ina viongozi na yuko Rais ambaye ndiye mwenye jukumu, kama hivyo basi tutulie tusubiri taarifa ya tume ili itupe mwelekeo wa namna ya kuiponya nchi,” amesema Mzava.
Katika maelezo yake hayo, amenukuu kauli iliyowahi kutolewa na Rais Samia, “yaliyotokea Oktoba 29, 2025 siyo mambo mazuri, nitoe pole kwa waliopoteza mali na ndugu zao na kama Taifa tunaendelea kuvuka salama.”
Ametumia jukwaa hilo, kuwaomba wabunge kushikamana kwa lengo la kuisaidia nchi kwenye ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.6 hadi saba.
Hoja kuhusu tukio hilo, ilitolewa pia na mbunge wa Bunda Mjini (CCM), Ester Bulaya aliyesema kama Taifa lilishakubali kuwa yaliyotokea Oktoba 29 siyo mazuri, ni vema Watanzania wakakubaliana kuwa siyo mambo mazuri.
“Tulikuabaliana yaliyotokea sio mazuri, Rais ameonesha nia ya kutatua na amesema bayana tume ikileta majibu kama kuna taasisi ilifanya makosa itawajibika, tumuunge mkono ili Taifa likimbie kimaendeleo kwa kuwa Taifa litakuwa moja,” amesema.
Ameunga mkono hoja ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuhusu watendaji wazembe wasifumbiwe macho, akiwataka wabunge washikamane kusimamia hilo ili kuhakikisha watumishi wazembe wanachukuliwa hatua.
Mbunge mwingine aliyezungumzia jambo hilo ni, Ezra Chiwelesa wa Biharamlo Magharibi, aliyetoa pole kwa kadhia iliyotokea Oktoba na akaomba hatua stahiki zichukuliwe kwa waliohusika.
“Tumeona mheshimiwa Rais amefanya juhudi kubwa ya kurudisha Taifa, madhila haya yametokea kwenye maeneo yetu na aliahidi vijana waliokamatwa waachiwe na wameachiwa, hivyo tunampongeza Rais.
“Rais aliahidi kuunda kuunda Tume na ameunda na sasa wanachukua maoni kwa wananachi, amezungumza na mabalozi na kila jambo linakwenda vizuri kwa sasa tuwe wavumilivu mama yuko kazini,” amesema.
Wakati mbunge huyo akichangia, alisimama mbunge mwingine ambaye hakutambulishwa jina lake akaomba kutoa taarifa na alipopewa nafasi na Naibu Spika, alisema mbunge huyo anapotosha kwa kuwa, siyo wote walioko gerezani kutokana na sakata la Oktoba 29, kwamba wametoka.
Taarifa hiyo ilikataliwa na Chiwelesa na akaendelea na mchango wake, kwa kueleza utekelezaji wa ahadi za Rais ndani ya siku 100 ikiwamo bima ya afya kwa wote, akiomba Serikali iongeze idadi ya watu kwenye kifurushi badala ya sita kama ilivyopendekezwa kwa kuwa, watu wa vijijini ni wengi.
Akiwasilisha hoja ya azimio la kujadili hotuba hiyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu amesema Serikali imeweka mkazo kwenye uwajibikaji na uadilifu ili kuhakikisha wananchi wananufaika na kupata huduma zinazostahili.
Amesema Serikali haitawavumilia viongozi wanaotoa visingizio na wasiowajibika na kutoa majibu ya ujanjaujanja kwa wananchi badala yake, kila mmoja atimize wajibu wake kulingana na eneo alilokabidhiwa.