Hatua hiyo imewalazimisha watoto hao kukabiliana na taratibu tata za uhamiaji bila msaada wa wakili, hali ambayo wataalamu wanasema ni ukiukwaji wa moja kwa moja wa haki za mtoto na inaweka hatarini usalama, ustawi na mustakabali wao.

Kuwanyima watoto haki yao ya uwakilishi wa kisheria na kuwalazimisha kupitia taratibu tata za uhamiaji bila msaada wa mwanasheria ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto,” wamesema wataalamu hao.

Chini ya sheria ya uidhinishaji upya wa kulinda waathirika wa biashara baramu ya Binadamu ya mwaka 2008 (TVPRA), Ofisi ya Makazi ya Wakimbizi (ORR) ina wajibu wa kuwatunza na kuwalinda watoto wasiokuwa na waandamani. Sheria hiyo pia inaitaka Idara ya Usalama wa Ndani (DHS) kuwalinda watoto dhidi ya manyanyaso, unyonyaji na biashara haramu ya binadamu. TVPRA inahakikisha kuwa watoto hawa wanapata msaada wa kisheria na hawapaswi kufukuzwa kwa taratibu za haraka (expedited removal).

Hata hivyo, tarehe 18 Februari 2025, idara ya mambo ya ndani ya Marekani iliagiza mashirika yasiyo ya kiserikali kusitisha kazi na ikasitisha ufadhili wa mawakili waliokuwa wakiwawakilisha watoto hawa, hali iliyopelekea kusimamishwa kwa mpango wa watoto wasiokuwa na waandamani. Ingawa kesi zimefikishwa mahakamani kupinga uamuzi huo, watoto takriban 26,000 waliathirika, wengi wao wakipoteza msaada wa kisheria na kubaki katika hatari ya kufukuzwa kwa nguvu licha ya kustahili hifadhi au msaada wa kisheria.

Ripoti hizi pia zinaeleza kuwa watoto wanazuiliwa katika seli zisizo na madirisha, wananyimwa huduma stahiki za afya, na hutenganishwa na wazazi au walezi kwa muda mrefu. Kati ya Januari na Agosti 2025, muda wa wastani wa watoto kukaa kizuizini uliongezeka kutoka takriban mwezi mmoja hadi miezi sita, huku idadi ya watoto waliokuwa wakiachiliwa kwa walezi wa kifamilia ikishuka kutoka karibu asilimia 95 hadi asilimia 45.

Wahamiaji kutoka Amerika ya Kati wanapumzika kwenye kituo cha muda mpakani mwa Mexico na Marekani.

© UNICEF/Adriana Zehbrauskas

Wahamiaji kutoka Amerika ya Kati wanapumzika kwenye kituo cha muda mpakani mwa Mexico na Marekani. (Maktaba)

Wataalamu  wamesema kumekuwa na taarifa za mara kwa mara za kufukuzwa kinyume cha sheria kwa watoto wasiokuwa na waandamani, kinyume na kanuni ya kutorejesha mtu mahali atakapopata madhara (non-refoulement), ikiwemo watoto waathirika wa biashara haramu ya binadamu au walio katika hatari ya kunyonywa.

Pia imeripotiwa kuwa watoto wanalazimishwa kuchagua kati ya kupokea dola 2,500 ili kujiondoa wenyewe nchini, hatua inayowanyima ulinzi wa kisheria chini ya TVPRA, au kukabiliwa na kizuizi cha muda usiojulikana na kuhamishiwa kwa mamlaka ya uhamiaji (ICE) wanapofikisha umri wa miaka 18.

Taratibu za haki zinazozingatia maslahi ya mtoto zinapaswa kuhakikishwa katika kesi zote za uhamiaji na hifadhi zinazohusisha watoto,” wamesema wataalamu hao.

Wamesisitiza kuwa watoto wanapaswa kuwa na haki ya kukata rufaa au kufungua mashauri ya kiutawala na mahakamani dhidi ya maamuzi yanayowaathiri wao au wazazi/walezi wao, na kwamba ni lazima kuepukwa kwa ucheleweshaji wa taratibu unaoweza kuathiri vibaya haki zao.

Wataalamu wameongeza kuwa taratibu za haraka zinapaswa kutumika tu pale zinapozingatia maslahi bora ya mtoto na bila kukiuka haki za msingi za mwenendo wa haki. Pia wamesema kuwa wanaendelea kuwasiliana na Serikali ya Marekani kuhusu masuala haya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *