Akikumbuka miaka 81 tangu kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz-Birkenau, Guterres amesema “siku hii inahitaji tafakuri ya kina na dhamira isiyotetereka kukabiliana na chuki na kulinda haki za msingi”.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres anazungumza katika sherehe ya Ukumbusho wa Maangamizi Makubwa ya Watu wa Umoja wa Mataifa, ambayo huadhimishwa siku ya kimataifa ya kuwakumbuka waathiriwa.
Ameongeza kuwa “Tunawaheshimu na kuwaenzi waathiriwa wa mauaji ya kimbari ya Holocaust, kwa kukataa kusahau mauaji hayo na kwa kusimama kidete dhidi ya kila aina ya kudhalilisha utu.”
Maisha milioni sita, sio takwimu tu
Katika ujumbe wake wa siku hii , Katibu Mkuu amekumbusha kuwa mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa na utawala wa Nazi yalisababisha kuuawa kwa Wayahudi milioni sita, pamoja na watu wa Roma na Sinti, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyoteswa.
Alisisitiza uhalisia wa kibinadamu ulio nyuma ya takwimu hizo, akisema, “Kila mhanga alikuwa na jina, matumaini na ndoto. Kila mmoja alinyimwa na kuharibiwa haki zake kwa utaratibu.”
Guterres ameongeza kuwa Holocaust haikuwa tukio lisiloepukika, akionya kwamba “waliopanga mauaji walieleza wazi nia zao, na chuki na vurugu zilijitokeza hadharani.”
Dalili za hatari katika dunia ya leo
Guterres ameonya kuwa chuki dhidi ya Wayahudi, ubaguzi wa rangi na kutovumiliana vinaendelea kuchochewa na “lugha za kudhalilisha utu na kutojali, ikiwemo katika majukwaa ya kidijitali”.
Hivyo amesisitiza “Lazima tuchukue msimamo thabiti kuheshimu waathiriwa wa zamani na kuzuia uhalifu mpya,” amesema, akihimiza jamii kukataa chuki na dhuluma popote vinapojitokeza kwa kuwa kumbukumbu lazima ziandamane na hatua za kulinda utu wa binadamu leo.
Sala na ukimya wakati wa Ukumbusho wa Siku ya Kimataifa ya Kukumbuka Waathirika wa Maangamizi Makubwa ya Watu wa Umoja wa Mataifa
Manusura watoa shuhuda Makao Makuu ya UN
Maadhimisho ya kumbukumbu ya siku hii katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York yamejumuisha ushuhuda wa manusura wa mauaji hayo ya kimbari ya Holocaust, Sara Weinstein na Blumenthal Lazan, pamoja na hotuba za maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa dunia.
Simulizi za manusura hao zimegeuza historia kuwa uzoefu halisi wa maisha, zikikumbusha wajumbe kwenye ukumbi wa Baraza Kuu kwamba mauaji ya Holocaust yalianza kwa maisha ya kawaida yaliyovunjwa ghafla na chuki na ubaguzi ulioratibiwa na dola.
“Mama yangu aliniokoa kwa kuweka rehani uhai wake”
Sara Weinstein amesimulia kuishi katika ukatili wa hali ya juu baada ya kutoroka kutoka geto akiwa mtoto.
Baada ya kusalitiwa alipokuwa mafichoni, alinusurika mauaji ambapo mama yake aliuawa akimlinda. “Utoto wangu uliishia katika vurugu na hofu,” amewaambia wahudhuriaji wa kumbukumbu hiyo, akieleza miaka aliyokaa msituni akihangaika kwa njaa na baridi bila viatu.
Weinstein ameonya kuwa Holocaust “haikuanza na vyumba vya gesi, bali ilianza na kauli, chuki na hali ya kutojali,” akitoa wito wa kuwa macho kwa chuki dhidi ya Wayahudi inayoendelea hii leo.
Rais wa Mkutano Mkuu Annalena Baerbock anazungumza kwenye Sherehe ya Ukumbusho wa Holocaust ya Umoja wa Mataifa, iliyofanyika kuheshimu siku ya kimataifa ya kukumbuka waathirika.
Kuishi kupitia ujasiri na ukimya
Blumenthal Lazan manusura mwingine wa mauaji ya Holocaust ameelezea utoto wake uliogubikwa na sheria za Nuremberg, Kristallnacht na maisha katika kambi za mateso nchini Ujerumani na Uholanzi.
Amesema aliishi kwa sababu ya uthabiti, nidhamu na ujasiri wa mama yake. “Wakati mwingine ukimya uliokoa maisha,” amesema, akikumbuka jinsi kujidhibiti kulivyokuwa suala la uhai au mauti katikati ya hofu ya kila siku. Ameongeza kuwa ukombozi ulifika kwa gharama kubwa, ikiwemo kifo cha baba yake muda mfupi baadaye.
Wito wa kulinda ubinadamu wa pamoja
Licha ya mateso makubwa, wanawake hao wawili waliijenga upya maisha yao na kujitolea kwa elimu na kumbukumbu.
Ushuhuda wao umeakisi dhamira ya msingi ya Umoja wa Mataifa, ulioanzishwa baada ya maafa ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia na Holocaust.
Akisisitiza urithi huo, Guterres amesema kuwaheshimu waathiriwa kunamaanisha “kuthibitisha ubinadamu wetu wa pamoja, kulinda utu wa binadamu, na kutetea maadili yanayounganisha jumuiya ya kimataifa,” ili uhalifu kama huo asilani usirudiwe tena.