
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameeleza umuhimu wa hatua hii akisema: “Chakula wanachokula watoto shuleni, na mazingira yanayochochea wanachokula, vinaweza kuwa na madhara makubwa katika ujifunzaji wao, na hata kwa afya na ustawi wao kwenye maisha yao yote.”
Takwimu za hivi karibuni za mwaka 2025 zinaonesha kuwa takriban mtoto mmoja kati ya kumi wenye umri wa kwenda shule anaishi na unene uliopitiliza, idadi ambayo sasa imevuka ile ya watoto wenye uzito mdogo. Shule zimekuwa zikishuhudia ongezeko hili la uzito uliopitiliza huku utapiamlo ukiendelea kuwa changamoto inayodumu. Dkt. Tedros ameongeza kuwa: “Kupata lishe sahihi shuleni ni muhimu sana kwa kuzuia magonjwa ya baadaye maishani na kutengeneza watu wazima wenye afya bora.”
Uboreshaji wa vigezo vya chakula shuleni
Katika mwongozo huo, WHO imependekeza kuwekwa kwa sheria na vigezo maalum vitakavyoongeza upatikanaji wa vyakula na vinywaji vyenye afya huku vikidhibiti vile visivyofaa. Hatua hizi ni pamoja na kutumia mbinu za ushawishi kama vile kubadilisha namna chakula kinavyowekwa, bei, au uwasilishaji wake ili kuwatia moyo watoto kuchagua chaguzi bora zaidi. Inakadiriwa kuwa watoto milioni 466 wanapata milo shuleni kote duniani, lakini taarifa kuhusu ubora wa lishe ya vyakula wanavyopewa bado zimekuwa chache kwa muda mrefu.
Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa sera pekee hazitoshi bila kuwepo kwa mifumo imara ya ufuatiliaji na usimamizi ili kuhakikisha miongozo hiyo inatekelezwa kikamilifu na kwa msimamo. Hadi kufikia Oktoba 2025, ni nchi 104 pekee wanachama ambazo zimekuwa na sera za afya ya chakula shuleni, na ni nchi 48 pekee ambazo zimeweka vikwazo dhidi ya matangazo ya vyakula vyenye sukari, chumvi, au mafuta mengi.
WHO imeahidi kuendelea kutoa msaada wa kitaalam na kubadilishana maarifa na nchi wanachama ili kusaidia watoto kukua katika mazingira yanayozingatia afya.