
Mtaalamu wa kijeshi wa ndege zisizo na rubani ameonya kuwa, utitiri wa ndege zisizo na rubani za Iran ni “tishio halisi” kwa vyombo vya jeshi la wanamaji la Marekani vyenye thamani kubwa, wakati huu ambapo Washington inaripotiwa kuwa inaendelea kujizatiti kijeshi katika eneo la Asia Magharibi.
Cameron Chell, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi mwenza wa Draganfly, kampuni ya ubunifu na utengenezaji wa ndege zisizo na rubani, ameiambia tovuti ya Fox News Digital kwamba, kuongezeka uimarikaji wa Jamhuri ya Kiislamu kwenye mifumo ya ndege zisizo na rubani kunaweza kutumika ili kushadidisha mashambulizi dhidi ya vyombo vya majini vya Marekani kama vile manowari ya USS Abraham Lincoln.
“Uwezo wa Iran wa kutumia ndege zisizo na rubani umegharimu mamilioni ya dola,” ameeleza Chell na kuongezea kwa kusema: “Iran imeanzisha mfumo wa tishio lenye athari za pande kadhaa dhidi ya mifumo ya kijeshi ya kisasa zaidi.”
Mtaalamu huyo wa masuala ya kijeshi amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaweza kurusha idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani moja kwa moja kulenga vyombo vya majini na kufafanua kwa kusema: “ikiwa mamia yatarushwa ndani ya muda mfupi, baadhi yake yana uhakika wa kupenya. Mifumo ya kisasa ya ulinzi haikuundwa hapo awali kukabiliana na aina hiyo ya mashambulizi ya mmiminiko. Kwa vyombo vya majini vya juu ya bahari vya Marekani vilivyoko karibu na Iran, manowari zitakuwa ndiyo walengwa wakuu.”
Huku akitahadharisha kwamba droni za Iran ni tishio la uhakika kwa vyombo vya majini vilivyoko juu ya bahari, Chell amesema: “vyombo vya Marekani katika eneo ni vikubwa, vinasonga polepole, na vinagundulika kirahisi kwenye rada, jambo linalovifanya viwe rahisi kulengwa.”
Sambamba na hayo, kamanda mwandamizi wa jeshi la Iran ameapa kwamba Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali na la haraka kwa vitisho na matamshi ya Marekani, akirudia matamshi yaliyotolewa na maafisa mbalimbali wa Iran kuhusu uwezekano wa kuanzishwa chokochoko mpya za kijeshi na Washington.
Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi, kamanda wa Kitengo cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ametoa matamshi hayo kando ya mkutano wa makamanda wa zamani na wa sasa wa IRGC uliofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Walinzi wa Kitaifa.
“Trump anazungumza sana, lakini anapaswa kuwa na uhakika kwamba atapokea jibu lake kwenye medani,” amesisitiza Jenerali Mousavi…/