Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekosoa vitisho vya kijeshi vya mara kwa mara vya Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Iran, ambapo hivi karibuni alitishia Iran kwa kisingizio cha miradi ya nyuklia ya nchi hiyo. Wamesema kuwa Israel inaiburuta Washington katika vita vingine kwa ​​niaba ya serikali ya Tel Aviv.

Katika chapisho alilotuma katika mtandao wa Truth Social jana Jumatano, Trump alisema kuwa, “muda unayoyoma kufikia mapatano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran” na kutahadharisha kuwa: Shambulio lijalo “litakuwa baya zaidi” kuliko lile lililofanywa katika msimu wa joto uliopita, wakati jeshi la Marekani liliposhambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran sambamba na mashambulizi ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Trump aliandika: Msafara wa meli zinazoongozwa na manowari ya USS Abraham Lincoln ni mkubwa kuliko ule uliotumwa Venezuela, kabla tu ya nchi hiyo kushambuliwa kijeshi, hatua iliyopelekea kutekwa nyara  Rais Nicolas Maduro mapema mwezi huu. 

 Trump amekuwa akitoa vitisho vya kuishambulia kijeshi Iran baada ya  maandamano ya hivi karibuni kuhusu masuala ya uchumi. Maandamano hayo ya wananchi yalitekwa nyara na mamluki na magaidi waliokuwa na silaha wenye uhusiano na mataifa ya kigeni.

Gerald Celente mtabiri mtajika wa masuala mbalimbali Marekani ameandika katika mtandao wake wa kijamii wa X kwamba Trump ataitumbukiza Marekani katika vita na Iran kwa lengo la kupotosha umma kuhusu hali mbaya inayoisumbua Marekani. Aliongeza kuandika: “Ni rahisi, Trump ameshindwa.” 

Naye Luteni Kanali Daniel Davis veterani wa vita amesema kuwa jeshi la Marekani liko mikononi mwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel. Ametahadharisha kuwa: Wachochezi wa vita kama Netanyahu na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo wanaiburuta Marekani kwenye janga.

 Cenk Uygur, mkurugenzi wa mtandao wa TYT wa Marekani kwa upande wake amesema kuwa Israel inabeba dhima kwa Mmarekani yeyote atakayepoteza maisha kufuatia uvamizi wowote wa kijeshi utakaoanzishwa na Marekani dhidi ya Iran.

Wakati huo huo, mwandishi wa habari wa Uingereza aliyeshinda tuzo ya uandishi wa habari, Afshin Rattansi ameorodhesha matamshi ya wachambuzi waliosema Israel inataka vita kati ya Wairani na Wamarekani. 

Rattansi  ameandika: ‘John Mearsheimer amesema: ‘Iran na Marekani hawataki kupigana. Ni Waisraeli ambao wamekuwa wakijaribu kuwatumbukiza Wairani na Wamarekani katika mapigano.’

Vilevile amemnukuu Profesa Jeffrey Sachs akisema: ‘Ndoto ya Netanyahu maishani ni kuona vita vikitokea kati ya Marekani na Iran.’

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *