
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa Tehran iko tayari kwa vita na mazungumzo lakini haitakubali kuwekewa masharti. Araqchi ameeleza haya kufuatia vitisho vya kijeshi vya Washington dhidi ya Tehran.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari huko Ankara, Uturuki akiwa pamoja na mwenyeji wake, Hakan Fidan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: Iran iko tayari kuingia katika mazungumzo ya nyuklia ikiwa yatafanyika kwa usawa, kwa kuzingatia maslahi ya pande zote na kuheshimiana.
“Ikiwa mazungumzo ni ya haki, Iran iko tayari kushiriki katika mazungumzo na madajiliano. Hatutakubali kwa njia yoyote kushurutishwa na kushinikizwa.” amesema Sayyid Abbas Araqchi.
Ameongeza kuwa, amefurahi kufanya ziara Uturuki na ametaja mazungumzo kati yake na Fidan kuwa chanya na yenye manufaa. Amesema, Iran na Uturuki ni majirani na marafiki ambao wamekuwa bega kwa bega katika siku za dhiki na faraja.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Iran inaunga mkono ubunifu wowote kwa ajili ya amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia na kuzima njama mbovu za Israel.
Akijibu maswali kuhusu kuwasiliana na Washington, Araqchi amesema: Serikali ya Marekani imetaka mazungumzo kupitia wasuluhishi mbalimbali. “Iran haina tatizo na mazungumzo. Lakini mazungumzo hayawezi kufanyika mkabala wa vitisho. Wanapaswa kuachana na vitisho na kuwa tayari kwa mazungumzo ya haki.”
“Iran haijawahi kuacha diplomasia na kamwe haitaiacha,” alisisitiza mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesisitiza kuwa Ankara inapinga hatua za kijeshi dhidi ya Iran na kwamba masuala ya ndani ya Iran yanapasa kutatuliwa kwa amani na wananchi wa Iran bila ya kuingiliwa na mataifa ya kigeni.